November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Dkt. Nchemba atoa maelekezo PPRA

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

Waziri wa Fedha Dkt Mwigulu Nchemba 
amezielekeza taasisi zote za umma kuzingatia matakwa ya sheria ya ununuzi wa umma, na kutumia Mfumo wa NeST ili kuongeza ufanisi na kuhakikisha tunapata thamani halisi ya fedha.

Dkt Nchemba aliyasema hayo septemba 28 jijini Dar es Salaam wakati alipokuwa akipokea ripoti ya mwaka ya utendaji wa Mamlaka hiyo ya mwaka 2023/24, ambapo alisema endapo watakuwa na changamoto yoyote wanapaswa kuwasiliana na PPRA ili wapate maelekezo na idhini ya hatua zinazopaswa kuchukuliwa.

Amesema sheria imeweka kosa la jinai kwa mtu ambaye kwa makusudi ataamua kufanya ununuzi nje ya Mfumo wa kielektroniki hivyo mtu huyo akibainika na kuthibitika atapata adhabu ikiwa ni pamoja na kifungo cha miaka mitatu jela.

“Nimesikia kuwa zipo baadhi ya taasisi nunuzi bado zinasitasita kutumia Mfumo wa NeST ingawa zimewezeshwa kuutumia Mfumo. Nazielekeza taasisi zote za umma kuzingatia matakwa ya sheria ya ununuzi wa umma, na kutumia Mfumo wa NeST ili kuongeza ufanisi na kuhakikisha tunapata thamani halisi ya fedha. Na endapo watakuwa na changamoto yoyote wanapaswa kuwasiliana na PPRA ili wapate maelekezo na idhini ya hatua zinazopaswa kuchukuliwa.”

Aidha Dkt. Nchemba aliiagiza Mamlaka ya Ununuzi wa Umma ( PPRA) kuhakikisha inayaendeleza mafanikio waliyoyapata kwa mwaka uliopita ili Mamlaka hiyo iendelee kukua kila mwaka na  kuitaka Mamlaka hiyo kubuni vyanzo mbalimbali vya fedha ili kuweza kukabiliana na changamoto ya upungufu wa bajeti.

“Naoielekeza Bodi na Menejimenti ya PPRA kuhakikisha mafanikio mlioyapata yanadumishwa na tuone ukuaji wa Taasisi hii kila mwaka ili kuwapa ahueni watoa huduma na wananchi kwa ujumla. Aidha, hakikisheni misingi ya uadilifu, uwajibikaji na kufuata sheria inaimarishwa ili kujenga Taasisi yenye tija na heshima katika bara la Afrika.” 

Aidha  Waziri Nchemba aliielekeza taasisi nunuzi kuzingatia sheria, lakini pia kuunga mkono juhudi za kuwainua watanzania ambao wana hali za kati na za chini kiuchumi ili washiriki keki ya Taifa.

Pia aliiagiza PPRA kuendelea kutoa elimu kwa umma ili kila mtumiaji wa Mfumo awe na uelewa na waweze kuufahamu mfumo huo wauunge mkono na kuhamasika kujisajili kama wazabuni kushiriki michakato ya ununuzi wa umma.

“Naielekeza PPRA kuendelea kutoa mafunzo kadiri inavyotakiwa, ili kila mtumiaji wa Mfumo awe na uelewa. Pia, kuongeza nguvu katika kutoa elimu kwa umma na uhamasishaji kwa watanzania ili waweze kuufahamu huu Mfumo, wauunge mkono na kuhamasika kujisajili kama wazabuni kushiriki michakato ya ununuzi wa umma. Hii ni kwa kuzingatia kuwa fursa za upendeleo zilizotolewa na Sheria ya Ununuzi wa Umma kwa watanzania hawawezi kuipata kama hawatakuwa wamejisajili kwenye Mfumo huu wa NeST.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi PPRA Dkt. Leonada Mwagike alisema kuwa pamoja na mafanikio mengine, Mamlaka ilifanikiwa kuokoa Jumla ya shilingi 14.94bn/- kupitia ukaguzi na shilingi  2.7tril/- kupitia ufuatiliaji ambapo amesisitiza ili kuendelea kudhibiti upotevu wa fedha za miradi, Mamlaka itaendelea kuzichukulia hatua za kisheria taasisi zote ambazo hazitumii mfumo wa NeST katika ununuzi.

Mfumo wa NeST ulianza kufanya kazi Julai 2023 ukilenga zaidi kusaidia kudhibiti matumizi ya fedha za serikali hasa kwenye utekelezaji wa miradi.