December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Dkt. Mabula atoa onyo kwa viongozi wanaogawa Ardhi kinyume na sheria

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

Viongozi wote nchini wa vijiji na vitongoji na wale wa serikali za mitaa ambao wanachukua madaraka ya kugawa ardhi kinyume na taratibu za sheria, wametakiwa kuacha maramoja kujivika madaraka ya kuvunja sheria za ardhi na kusababisha uvamizi kwenye maeneo yenye milki za watu

Agizo hilo limetolewa leo (Agosti 10, 2022) na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula wakati akiwasilisha taarifa kwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge ili kushughulikia wananchi wote ambao wamekuwa wakikiuka maadili ya kuvunja sheria na kusababisha migogoro ambayo imekuwa ikileta maumivu makubwa kwa wananchi.

Waziri Dtk. Mabula amesema imebainika kwamba kero nyingi zinasababishwa na viongozi ambao wananchi wamewaamini na kuwapa madaraka ya kuwaongoza;

“Kumekuwa na wimbi kubwa sana la wenyeviti wa vijiji na vitongoji kujivika madaraka yasiyowahusu hasa katika kugawa ardhi ambayo ipo chini ya sheria nyingine, viongozi hawa baadhi yao wamekwenda mbali kiasi cha kudiliki kugawa ardhi zenye hati miliki.”Amesema Waziri Mabula na kuongeza kuwa

“Mwenyekiti wa kijiji huna mamlaka yoyote ya kuingilia kugawa ardhi ambayo ipo chini ya sheria nyingine isipokuwa kwa kufuata taratibu.”

Pia Waziri Dkt. Mabula amesema Katika eneo la Mapinga baadhi ya Watu wametengeneza makundi ya uhalifu ambayo yanauza na kuingia kwenye maeneo ya Watu kwa kutumia nguvu, hivyo amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa pwani kuwashughulikia kwa kuchukua sheria stahiki;

“Magenge haya yanajulikana na yamefikia hatua ya kujeruhi Watu na yanaendelea kutishia Watu bila kuchukuliwa hatua hivyo mkuu wa mkoa Watu hawa washughulikiwe kwa sheria kama ambavyo zinatajwa”

“Baadhi ya Watu waliotajwa sana na wananchi mbele ya kamati kwamba wanahusika na magenge hayo ya uhalifu wa kuvamia ardhi wanajulikana na kamati na imewaorodhesha” Alisema Waziri Mabula

Kwa upande Mwingine Waziri Dkt. Mabula amesema imebainika kuwa wapo wananchi ambao wameuza maeneo yao kwa zaidi ya mtu mmoja kwa kutumia mahudhurio waliyotumia kumuuzia mtu mwingine ambapo vitendo hivyo hufanywa na viongozi wa vijiji na vitongoji ambao wamethibitika kugawa na kuthibitisha mauziano ya eneo moja kwa zaidi ya mtu mmoja na huku wakifaidi fedha kwa ugawaji ambao wamekuwa wakiufanya;

Pia Waziri Dkt. Mabula amesema Wizara itaendelea kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mashamba pori ambayo yameonekana Watu wamemilikishwa lakini hawayaendelezi.

Waziri Dkt. Mabula amewataka wananchi kutonunua eneo bila kufuata taratibu zinazotakiwa hasa kwa kufika kwenye mamlaka husika kujiridhisha kama anayeuza ni mmiliki halali na kuwa na nyaraka za eneo husika.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amesema suala Kubwa waliloliona ni Watu kutoheshimu sheria, ambapo nchi inaendeshwa kwa mujibu wa sheria hivyo ameahidi kusimamia utekelezaji kama ambavyo maelekezo yatakavyotoka;

“Tutasimamia utekelezaji kama ambavyo maelekezo yatakavyotoka kuhakikisha tunaachana na migogoro hii ili Watu waweze kuishi kwa amani, wafanye shughuli za maendeleo na mkoa wetu uweze kupiga hatua”

Pia RC Kunenge alimuhakikishia waziri Mabula, kutokomeza migogoro ya ardhi na changamoto nyingine katika mkoa wao

Aidha Rc Kunenge amesema Mkoa wa pwani ni mkoa wenye fursa nyingi lakini changamoto kubwa waliyonayo ni migogoro ya Ardhi ambapo mwaka 2021 wananchi walieleza kero zao na baada ya kero hizo ilionekana kuna haja ya kufanya kazi ya ziada na yenye umakini mkubwa ili kutenda haki.

“Mwaka 2021 Tulizundua kampeni rasmi ya tokomeza migogoro ya Ardhi mkoa wa pwani na hii leo ni sehemu ya utekelezaji wa kampeni hiyo na ilikupendeza Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi uliunda timu ya wataalamu ambapo walipata nafasi ya kuja Mapinga na kuwasikiliza wananchi lakini leo umekuja kutoa mrejesho wa kero walizozieleza wananchi”

Naye Kamishna Msaidizi wa Polisi Makao Makuu Upelelezi na Mwenyekiti wa Kamati Usuluhishi Ardhi Mapinga, Peter Matagi, amesema watu wengi wamejipatia pesa kwa njia ya udanganyifu kwenye maeneo ya Watu ambao wana hati miliki hivyo amemuomba waziri kulifanyia kazi kwa undani zaidi suala hilo.

“Nchi hii inaenda kwa utii wa sheria bila shuruti , Watu wangefatisha sheria nina hakika haki za Watu zisingepotea, Viongozi wetu tunaowateua kuanzia ngazi ya watendaji wa vijiji wamekua chachu ya migogoro kwa mkoa wa pwani ikiwemo kuuza viwanja bila kufuata utaratibu na kughushi nyaraka.”