January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Bashungwa aagiza wakurugenzi kujenga matundu ya vyoo kwenye shule kupitia fedha za ndani

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Innocent Bashungwa amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kutenga fedha na kuweka kipaumbele cha ujenzi wa matundu ya vyoo katika shule za msingi na sekondari kupitia fedha za mapato ya ndani ya halmashauri.

Ametoa maelekezo hayo leo Machi 28, 2022 wakati alipotembelea Shule ya Sekondari ya Bungene iliyopo Wilaya Karagwe mkoani Kagera na kukuta upungufu wa matundu ya vyoo ukilinganisha na idadi kubwa ya wanafunzi waliopo.

Mheshimiwa Bashungwa amesema, baada ya Mheshimiwa Rais kuelekeza fedha za mkopo wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) katika ujenzi wa madarasa 12,000 ambayo yamepunguza msongamano na wanafunzi kutembea mwendo mrefu, sasa changamoto imebaki kwenye upungufu wa matundu ya vyoo shuleni.

Waziri Bashungwa amesema, katika jitihada za kupunguza uhaba wa madarasa katika Shule ya Sekondari Bugene, Serikali italeta fedha za kujenga vyumba vya madarasa manne na kutenga bajeti ya kufanya ukarabati wa madarasa na mindombinu iliyochakaa.

Pia Waziri Bashungwa amesema, Serikali itatoa fedha kujenga bweni moja ili kupunguza upungufu wa mabweni mawili katika shule hiyo ya Sekondari ya Bugene.

Awali, Mkuu wa Shule ya Sekondari Bugene, Asia Rupia ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha Sekta ya Elimu, miundombinu mbalimbali na kugharamia elimu bila malipo ambapo shule inapokea shilingi milioni 20.1 kila mwezi.