December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Bashe: Rais Samia hana deni katika sekta ya kilimo

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Kahama

WAZIRI wa Kilimo, Hussin Bashe, amesema Rais Dk.Samia Suluhu Hassan hana deni kwa Watanzania katika sekta ya kilimo, hivyo watendaji wa Wizara wana wajibu wa kuhakikisha yote yanayofanywa na Serikali yanatekelezeka.

Amesema, Rais Dk. Samia anapambana usiku na mchana na hayupo tayari kuona sekta hiyo inatetereka, hali iliyo mlazimu kuongeza bajeti sekta ya kilimo kutoka sh. bilioni 294 mwaka 2022/2023 hadi shilingi Trilioni 1.24 mwaka 2023/2024.

Akizungumza katika ziara yake ya kikazi mkoani Shinyanga wilayani Kahama, Waziri Bashe alisema kazi iliyotukuka inayofanywa na Rais Dk.Samia inapaswa kuungwa mkono na watendaji wote.

“Rais Dkt. Samia hana deni wizara ya kilimo ana ipenda sekta hii amefanya mengi, lengo likiwa ni kutaka matokeo sekta ya kilimo, haijawahi kutokea bajeti kutoka shilingi bilioni 294 hadi shilingi Trilioni 1.24, sisi wasaidizi wake na watendaji tunao wajibu wa kufanya kazi usiku na mchana,”alisema Waziri Bashe.

Alitumia fursa hiyo, kuwafikishia salamu za Rais Dkt. Samia wakazi wa Kata ya Isagehe na kueleza kuwa dhamira yake ya kukuza kilimo ni ya kudumu na ataendelea nayo katika kuinua hali ya wakulima nchini.

Aliwataka wataalamu sekta ya kilimo ikiwemo maafisa kilimo na ugani kuishi vijijini kuhakikisha wanasaidia jamii waliyopo ili kuiwezesha sekta ya kilimo kuwa na tija na kuleta matokeo anayoyatarajia Rais Dk. Samia.

Pia ameiagiza Tume ya Umwagiliaji kuhakikisha mradi wa bwawa la umwagiliaji lililopo katika kijiji cha Malenge, Kata ya Isagehe lenye ukubwa wa mita za ujazo 600,000,wenye thamani ya shilingi bilioni 2.5 linajengwa.

Waziri Bashe pia amemshukuru Mzee Shija Lukinga ambaye ni mmiliki aliyetoa eneo lake la ardhi bure ili kupisha mradi huo. “Hii ni taswira chache ya Mzee Shija kujitolea na ni kipaji cha kipekee.Bwawa hili linufaishe wakulima 427, mifereji isakafiwe kwa hekta 400 zilizobaki, tutumie wataalamu wa ndani katika ujenzi wa bwawa, ujenzi wa ghala na kinu na jina la mradi kuanzia sasa lisajiliwe kwa jina la Shija kutoka jina la awali la Malenge,”amesema waziri Bashe

Bashe ameongeza kuwa, Tume itoe ushauri wa zana zinazohitajika katika uzalishaji ndani ya skimu hiyo.

“Mradi huu uwe na kilimo cha uhakika cha kuvuna hadi mara tatu kwa mwaka”, amesema Waziri Bashe.

Aidha, Waziri Bashe amewashukuru pia Kampuni ya Uchimbaji Dhahabu,Barrick kwa kuwezesha mradi huo. “Sisi kama Serikali tutakamilisha usakafiaji wa kilometa 12 zilizobaki na Serikali itajenga hekta 400 za tuta zilizobaki,” ameongeza.

Ameeleza eneo hilo kutajengwa Kituo cha zana za Kilimo na ujenzi wa maghala kwa ajili uhifadhi wa mpunga. “Ninamuomba Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha,kufanya kikao cha ujirani mwema na Mkuu wa Mkoa wa Tabora ili bonde la Manonga lilindwe kwa ajili ya miundombinu ya uzalishaji wa chakula badala ya kujenga nyumba za wakazi. Tulinde ardhi ya kilimo,” alisema Waziri Bashe.

Katika hatua nyingine Waziri Bashe ametembelea shamba la Serikali ya kijiji la Kisuke lililopo Kahama na kuitaka ofisi ya Mkurugenzi wa halmashauri na ofisi ya Mkuu wa Mkoa kuhakikisha eneo hilo linapimwa ili lipate hati na isome eneo la kilimo Isuke na wizara ya kilimo

Pia eneo hilo, litanufaika na mradi wa Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT), kwa watu wa kijiji na Bodi ya Pamba ifanye eneo hilo kuwa mradi mkubwa wa kuzalisha pamba.

“BBT hii wanufaika wawe ni wananchi kwa kukatiwa maeneo hivyo itakuwa bbt ya wananchi wa kisuke na Serikali tutasimamia mradi huo na bodi pamba ifanye uwekezaji ilete trekta na pawatila za kutosha na umwagiliaji wafanye utafiti wa ujenzi wa bwawa. Hivyo wataalamu wa Wizara,watu wa pamba, bbt, Asa, umwagiliaji muunde timu ya utafiti na Mkurugenzi zungumzeni na tarura barabara ya kuingia shambani ifunguliwe,wizara tutashirikiana mkihitaji,”amesema.

Kwa upande wa Meneja wa Mradi wa Tume ya Umwagiliaji Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Ebenezer Kombe amesema bwawa la Shija litakuwa na mifereji mikuu na midogo ya kuingiza maji mashambani yenye urefu wa jumla ya kilomita 13 na eneo litakalotengwa kwa ajili ya kunywesha mifugo.