January 5, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Bashe azindua kiwanda cha pamba kilichofufuliwa na TADB

a Mwandishi Wetu,TimesMajira, Online, Kahama

NAIBU Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amezindua Kiwanda cha Pamba
cha Kahama (KACU) kilichofufuliwa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo
(TADB) ambapo zaidi ya sh. bilioni 4.6 zimeshatolewa na benki.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo mjini hapa leo, Bashe amesema
kufufuliwa kwa kiwanda hicho ni dhamira ya kweli ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya John Magufuli ya kuinua na kuongeza
uzalishaji wa mazao yote ya kimkakati ikiwepo pamba.

“Kuzinduliwa kwa kiwanda hiki leo (jana) ina maana kubwa sana kwa
wakulima wa pamba kwa maeneo hayo kwani kitasaidia kuongeza uzalishaji wa pamba na kuwaongezea kipato wakulima wa zao hili,” amesema.

Amesema kutokana na umuhimu wa kiwanda hicho alilazimika kuhamishia ofisi yake TADB ili kuhakikisha zoezi la kukifufua kiwanda linakamlika kwa wakati na kuleta mapinduzi ya dhahabu nyeupe (pamba).

“Napenda kuchukua nafasi hii kuipongeza benki ya TADB na mabenki
washirika wake, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mrajisi wa Ushirika na
wengine kwa namna mlivyosimamia kukamilika kwa zoezi la kufufua
kiwanda hicho ambacho kitawanufaisha wakulima mkoani Shinyanga,’’
amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Japhet Justine
amesema sema uzinduzi wa kiwanda hicho cha pamba utaongeza tija kwa wakulima kwa kuwa bei ya pamba itaongezeka na kuwafanya wamudu gharama za maisha na kuchangia ukuaji wa pato la Taifa.

“Uzinduzi wa kiwanda hiki utaongeza uzalishaji wa pamba ambayo ni
malighafi muhimu kwa viwanda vya ndani, lakini thamani ya zao la pamba litaongezeka na kuzidi kutoa mchango wake katika ukuaji wa pato la Taifa na mkulima mmoja mmoja,” amesema Justine.

Justine amesema vyama vya ushirika kupitia vyama vya ushirika
wa kilimo na masoko (AMCOS) vinakopesheka na kutoa wito kwa wakulima kujiunga na navyo ili waweze kufaidika na huduma za benki yake kwa karibu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini (TADB), Japhet Justine (katikati) akijadiliana jambo na Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe (kushoto) kabla waziri huyo hajazindua Kiwanda cha Pamba cha Kahama (KACU) mjini Kahama mkoani Shinyanga jana ambapo Benki ya TADB imekifufua. Uzinduzi huo ulihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa, Zainab Telack na mamia ya wakulima. Na mpiga picha wetu.

“Sisi kama Benki ya Kilimo tunaamini kuwa kilimo kinakopesheka kwa
kuwa tumefanya hivyo sehemu mbalimbali ikiwemo hapa Kahama, tunatoa wito kwa wakulima kujiunga kwenye hizo AMCOS ili waweze kukopeshwa kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa zao la pamba,” amesema.

Aliongeza kuwa licha ya bei ya zao la pamba kushuka thamani tangu
kufungwa kwa kiwanda cha pamba cha Kahama kwa msimu wa 2013/14, sasa kufufuliwa kwa kiwanda hicho kutarejesha matumaini mapya kwa wakulima wa zao hilo mkoani Shinyanga.

“Mbali ya kufufua kiwanda hiki ambacho kilisimamisha uzalishaji wake tangu msimu wa 2013/14, tumefanya juhudi kubwa kurejesha uzalishaji wa zao hilo na kwa msimu huu tumenunua kilo ya pamba kwa shilingi kati ya 800 mpaka 920,” amesema na kuongeza kuwa hilo ni jambo la kujivunia hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali inatekeleza azma yake ya ujenzi wa viwanda.

Justine mbali ya kuzishukuru taasisi mbalimbali pamoja na wadau
waliochangia kukamilika kwa mpango huo, ameeleza kuwa kiwanda hicho kitawanufaisha wakulima zaidi 6,800 kutoka AMCOS 79 jambo ambalo litaongeza tija kwa wakulima na Taifa kwa ujumla.