Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
WAZEE wanaoishi jimbo la Ilemela wametakiwa kutumia maabara ya Wazee kwa ngazi za mitaa, kata hadi Wilaya kuwasilisha kero zao ili ziweze kupatiwa ufumbuzi kwa maendeleo yao, jimbo na Taifa kwa ujumla.
Wito huo umetolewa na mgombea Ubunge wa jimbo la Ilemela kupitia CCM wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Kawekamo ikiwa ni muendelezo wa mikutano yake ya kampeni ya kuomba ridhaa ya kuchaguliwa kwa awamu ya pili kuongoza wananchi hao.
Amesema, Serikali ya Awamu ya Tano imechukua hatua ya kulinda maslahi ya wazee ikiwemo kutoa huduma bure za afya na utoaji wa ruzuku kwa watu wasiojiweza kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini wa TASAF.
“Tutumie uwepo wa mabaraza ya wazee kwa ajili ya kumaliza kero zetu, Serikali ya Awamu ya Tano ni sikivu imetoa kipaumbele kwa wazee hata kwenye huduma za afya na pia katika awamu inayofuata ya TASAF hakuna mtu mwenye sifa ya kuingia kwenye mpango huu akarukwa,” amesema Dkt. Angeline.
Pia akizungumza wakati wa mkutano wake na wananchi wa Kata ya Buzuruga, Dkt. Angeline amewaahidi wananchi kushirikiana nao kwa utatu mtakatifu kujenga vyumba vya madarasa na ofisi ya walimu endapo watachagua viongozi wanaotokana na Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa nafasi ya urais, ubunge na udiwani.
“Milioni 146.5 zimetengwa kwa ajili ya kujenga vyumba hivyo vya madarasa ambapo viwili ni katika shule ya Msingi Nyambiti na chumba kimoja ni katika Shule ya Msingi Amani huku ujenzi wa ofisi ya waalimu itakuwa katika shule ya Msingi Nyambit kwani lengo la serikali ni kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia na kuhakikisha Wilaya ya Ilemela inaendelea kushika nafasi ya juu katika matokeo ya kitaifa,” amesema Dkt.Angeline.
Aidha amewahimiza vijana wa Jimbo la Ilemela ikiwemo wa Kata ya Nyakato, kuchangamkia fursa ya mikopo ya asilimia 10 ambapo kati yake 4 kwa wanawake 4 kwa vijana na 2 kwa walemavu inayotolewa na Halmashauri ili kujiletea maendeleo binafsi, jimbo na Taifa kwa ujumla.
Amesema, wakati anaingia madarakani mwaka 2015 jimbo la Ilemela kupitia Manispaa lilikuwa na uwezo wa kukopesha jumla ya milioni 216 na mpaka mwaka huu 2020 wamefanikiwa kuongeza fedha za mikopo kwa vijana, wakina mama na watu wenye ulemavu kufika shilingi bilioni 1.431.
Kwa upande wake Meneja kampeni wa CCM Jimbo la Ilemela, Kazungu Idebe amewaomba wananchi hao kuwaamini wagombea wa CCM kwa kuwapigia kura nyingi za ndiyo ifikapo Oktoba 28 ili iwe rahisi kutekeleza shughuli za maendeleo badala ya kusikiliza porojo za wagombea wasioitakia mema nchi na wapinga maendeleo.
Katibu wa CCM Wilaya ya Ilemela, Aziza Isimbula amewasihi wananchi hao kuchagua wagombea wa CCM kwa nafasi za Urais, Ubunge na Udiwani kwani ni wagombea wenye sifa, malengo na wanaongozwa na ilani iliobeba mustakabali wa maendeleo ya wananchi hao na taifa kwa ujumla.
More Stories
Muhoji Sekondari kumaliza changamoto ya umbali kwa wanafunzi Musoma vijijini
Tanzania mwenyeji mkutano wa nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika
TANESCO yarudisha shukrani kwa jamii