October 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Baadhi ya wazee katika Jimbo la Vunjo wakimkabidhi Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi Taifa,James Mbatia fomu ya kugombea nafasi ya ubunge katika Jimbo la Vunjo mara baada ya kupitisha mchango wa kiasi cha sh. 370,000.

Wazee Vunjo wasema wanamtaka Mbatia tena, wamchukulia fomu

Na Dixon Busagaga ,Moshi

Wajumbe wa mkutano Mkuu wa Chama cha NCCR-Mageuzi Jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro kwa kauli moja wamechanga fedha kiasi cha sh. 370,000 na kumchukulia fomu Mbunge wa jimbo hilo anayemaliza muda wake, Mhandisi James Mbatia kwa ajili ya kugombea ubunge kwa kipindi kingine.

Hatua hiyo ya wajumbe wapatao 1,500 kutoka kata 16 za jimbo hilo inatokana na ukimya uliokuwa umetanda kwa Mbunge huyo pamoja na tetesi za kuwa hagombei tena nafasi ya ubunge na badala yake anakusudia kugombea nafasi ya urais.

Wazee Ernest Kipokola,Julica Maliki na Elias Munuo wakizungumza kwa niaba ya wazee wenzao walimuomba Mbatia kutangaza nia ya kugombea ubunge katika Jimbo la Vunjo na baadae wakapitisha harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kuchukua fomu.

“Mheshimiwa Mbatia amekuwa akifanya mambo makubwa na mazuri ya maendeleo katika Jimbo la Vunjo ikiwemo kuboresha miundo mbinu ya barabara,shule pamoja na mengine mengi ambayo amefanya kwa kipindi cha miaka mitano,”amesema Julica.

”Ndugu Mbatia Wanavunjo tunakuhakikishia kuna wanachama zaidi ya 200 kwenye kata yetu wanasema uendelee na ubunge,tutakupa kura zote za ndio,mambo uliyoyafanya ni makubwa,”ameongeza Julica.

Baadhi ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama cha NCCR-Mageuzi Jimbo la Vunjo wakishiriki mkutano wa jimbo hilo.

Naye Elias Munuo amesema, wananchi katika Jimbo la Vunjo wamekuwa mashahidi kwa kazi ambazo zimekwisha fanyika huku akimuomba kutoelekeza mawazo yake katika kugombea nafasi ya urais na badala yake arejee jimboni kumalizia kazi alizokwisha zianza.

“Tunakuomba kwa heshima zote uchukue fomu na utuhakikishie unagombea ubunge jimbo hili,nia yetu tunataka tukuone ukiendelea na ubunge na yale yote ambayo hujamaliza uyamalizie,”amesema Munuo.

Kufuatia maombi hayo kutoka kwa wazee Mbatia ametangaza rasmi kugombea ubunge Jimbo la Vunjo na kuahidi kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha maendeleo ya jimbo hilo yanazidi kukua kwa kasi ambapo pia aliwaahidi kuwatumikia kwa nguvu zake zote.

”Kutoka sakafu ya moyo wangu ,nabeba dhamana ya kugombea ubunge wa jimbo hili la Vunjo,naahidi tutafanya kazi kwa pamoja usiku na mchana ili kutimiza yale yote ambayo mnayatamani yafanyike,”amesema Mbatia.

“Vunjo ni yetu na niahidi kuwa Vunjo yetu itaendelea kung’ara na yale machache ambayo hatukuyakamilisha kutokana na changamoto za hapa na pale tutaenda kukamilisha,”ameongeza Mbatia.