November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wazee 1000 kukatiwa bima Mbarali

Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbarali

KATIKA kuhakikisha wazee wanapata huduma za matibabu ya uhakika Mbunge mteule wa Jimbo la Mbarali mkoani Mbeya,Bahati Ndingo amehaidi kuwakatia bima za afya wazee 1000 wasiojiweza wilayani humo.

Amesema hayo leo wakati wa maadhimisho ya siku ya Wazee Duniani ambayo kiwilaya yamefanyika katika Kata ya Kongolo Mswiswi Kijiji cha Azimio Mapula.

Mbunge mteule Jimbo la Mbarali Bahati Ndingo akizungumza katika maadhmisho ya siku ya wazee duniani

Ndingo amesema kuwa mara baada ya kuapishwa Bungeni Jijini Dodoma atakamilisha zoezi hilo atalenga zaidi wazee wenye uhitaji mkubwa kwanza kwa kuwashirikisha maofisa maendeleo ya jamii kata katika kuwatambua na atachukua wazee 50 kwa kila Kata.

Ameeleza kuwa kwa mpango huo wa bima za afya kwa wazee ataanza kutoa bima 1000 kwa kuanzia kwasababu katika wilaya hiyo kuna kata 20 .

“Nitashirikiana na maofisa maendeleo ya jamii kata kwa kuhakikisha wanaenda kila kata kutambua wazee ambao hawana wasaidizi na wenye maisha duni ili kuwakatia bima,”amesema Ndingo.

Aidha amesema kuwa Desemba mwaka huu zoezi hilo la ukamilishaji wa bima litakuwa limekamilika kwa Wazee idadi hiyo ya wazee ambayo ni ya kuanzia.

Sanjari na hayo amesema kuwa pamoja na changamoto zilizopo za Wazee kumekuwa na jitihada za serikali za kuhakikisha wazipatia ufumbuzi.

Vilevile amesema kwa mujibu wa sensa iliyopita ya mwaka 2022 Wilaya ya Mbarali ina wazee 20,000 pia wamegundua kuna wazee zaidi ya 500 ambao wana hali ya chini ambao wanahitaji msaada hivyo kutokana na sara ya Rais Samia ni kuhakikisha kundi hilo linapata matibabu ambapo ni lazima wadau wajitokeze kusaidia.

Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Kanali Denis Mwila ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Mbarali amemshukuru Mbunge huyo kwa kuonesha upendo kwa wazee.

“Jambo hili si dogo wengi wetu tunafahamu suala la matibabu kwa Wazee ni muhimu hasa kwa umri waliofikia wanakuwa na maradhi ya mara kwa mara,”amesema Kanali Mwila.