November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wazazi wanaoficha watoto wenye ulemau kuchukuliwa hatua za kisheria

Na Esther Macha,Timesmajira,Online, Mbeya

KAIMU katibu Tawala  Mkoa wa Mbeya ,Vicent Mbua amesema  kuwa mzazi yeyote atakayebainika  kumficha ndani mtoto mwenye ulemavu atachukuliwa hatua kali za kisheria dhidi yake .

Amesema kuwa lengo ni kuhakikisha kuwa  watoto wenye ulemavu wote  wanapata haki ya elimu kama walivyo wengine na kuwaficha ndani .

Mbua amesema hayo juzi wakati wa maadhimisho ya siku ya watu wenye ulemavu duniani amabyo yalienda sambamba na mahafali ya watoto wenye mahitaji maalum waliohitimu mafunzo ya awali kuingia darasa la kwanza.

Hata hivyo Mbua amewataka  wananchi kutoa taarifa kwa serikali dhidi ya wale wote wanaowaficha watoto wenye ulemavu ndani.

Aidha ameshukuru shirika la CST kwa kujikita kuwasaidia watoto wenye ulemavu kwa kuanzisha shule yao yenye mahitaji maalum pamoja na kuendesha program mbalimbali zinahamasisha kuwapeleka watoto wenye ulemavu shuleni.

Amesema  serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya elimu kwa kuhakikisha inakuwa rafiki kwa watoto wenye ulemavu na kwamba utekelezeaji unaendelea hata sasa kupitia ujenzi wa vyumba vya madarasa baada ya fedha za Uviko 19 kutolewa na serikali mbalimbali nchini.

Kwa upande Mkurugenzi wa Child Support Tanzania (CST) Noela Msuya ameiomba Serikali kuhakikisha vyuo vyote  walimu vinatoa mafunzo maalum ya namna ya kufundisha watoto wenye mahitaji maalumu ili wanapohitimu wawe na ujuzi pamoja na utayari wa kufundisha kundi hilo kuliko ilivyo sasa ambapo hulazimika kupata mafunzo upya.

Msuya amesema licha baadhi ya vyuo vya walimu  kutoa mafunzo kwa ajili ya kuwafundisha watoto wenye mahitaji maalum lakini uhitaji ni mkubwa sana hivyo serikali haina budi kutoa mafunzo hayo kwa vyuo vyote vya walimu nchini ili kuwasaidia watoto wenye ulemavu kusoma kwenye mazingira mazuri kupitia program ya elimu jumuishi.

Aidha Msuya amesema kutokana na uhaba wa walimu wa kufundisha watoto wenye mahitaji maalum kupitia mpango wa elimu jumuishi CST imekuwa ikitoa mafunzo maalum kwa walimu namna ya kuwafundisha watoto hao.

“CST tumejikita kuwahudumia watoto wenye ulemavu nchini ni baada kuona wanapata vikwazo mbalimbali ikiwamo kufungiwa ndani na kukosa haki ya kupata elimu, matibabu na huduma nyingine kupitia program yetu ya peleka marafiki zangu wote shule tumeweza kuwafikia watoto wengi,”amesema  Msuya.

Ameongeza kuwa hadi sasa jumla ya watoto 600 wamefikiwa na program hiyo kupitia shule 30 za Msingi mkoani Mbeya na kwamba lengo lao ni kuzifikia shule zote nchini.

Mwalimu anayehudumia watoto wenye mahitaji maalum,  Shule Msingi Katumba II, Juma Said amesema CST imekuwa na mchango kubwa katika kutimiza ndoto za watoto wenye ulemavu.

Amesema  shule yao inafanya kazi kwa karibu na CST na kwamba wamekuwa wakipata msaada wa vitu mbalimbali ikiwamo ujenzi wa miundombinu madarasa pamoja na vifaa mbalimbali vya kufundishia na kujifunzia.

Amesema kutokana na maboresho ya miundombinu ya majengo na vifaa yanayotolewa na serikali kwa kushirikiana na wadau kama CST ongezeko la kudahili wanafunzi limekuwa likiongezeka mwaka hadi mwaka kutoka wanafunzi 50 hadi 70.