January 16, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wazazi wa Wanafunzi Sekondari ya Muhoji waamua kutoa chakula kwa watoto wao

Fresha Kinasa,TimesMajiraOnline,Mara.

WAZAZI wa Wanafunzi wa Kidato cha kwanza  katika shule ya Sekondari  Muhoji  Kata ya Bugwema  ambayo ni Sekondari  Mpya ya Kata hiyo katika Jimbo la Musoma Vijijini Mkoani Mara, wamekubaliana kuhakikisha wanachangia upatikanaji wa chakula cha mchana kwa wanafunzi wote kuwawezesha Watoto wao wasome kwa ufanisi. 

Sekondari hiyo ambayo ilianza kujengwa kwa kutumia nguvu za wanavijiji, Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini,baadhi ya Wazawa wa Kijiji cha Muhoji pamoja na Serikali kuu ambayo imechangia ujenzi wa Sekondari hiyo Shilingi Mil.75 imetajwa kuwa, iko  tayari kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Januari 15,2025 imebainisha hayo ambapo Wazazi hao wamekubaliana katika kikao kilichofanyika Kijijini hapo mambo manne.

Ambapo Jambo la kwanza ni Wazazi  kuchangia chakula Cha mchana kwa wanafunzi wote. Huku Jambo la pili likiwa ni Wazazi hao  kukubaliana  kuwa watanunua madawati ya watoto wao ambayo yanatengenezwa Kijijini hapo.

Jambo la tatu “Wazazi watahakikisha kuna uhusiano mzuri kati yao na Walimu, na Kati ya Wanafunzi na Walimu. Na Jambo la  nne Wazazi wataendelea kushirikiana vizuri na Serikali kuhakikisha Sekondari yao inatoa elimu kwenye mazingira mazuri yenye mafanikio mazuri.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo,  miundombinu ya awali tayari imekamilishwa,  ambapo ukamilishaji umefanywa kwenye vyumba vya madarasa, Ofisi za Walimu, Vyoo, maktaba na chumba vya matibabu.

Nao Wananchi wa Muhoji akiwemo Yunis Bwire ameshukuru kwa hatua hiyo kubwa ambayo amesema imechangiwa na Mbunge Prof. Muhongo kutoa hamasa kwa Wananchi kuchangia maendeleo, kutoa fedha zake binafsi,  Fedha za Mfuko wa Jimbo na kushirikiana vyema na Serikali kukamilisha shule hiyo.

“Tunafurahi kwa sababu tunatambua fika kuwa, ili Watoto wafanye vizuri katika masomo yao lazima wapate Chakula, kwanza itasaidia hata mahudhurio yao darasani na kuongeza umakini wanapofundishwa na Walimu.” amesema Yunis  Bwire.

Yunis ameongeza kuwa,  shule hiyo  itatatua changamoto kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza  kutembea umbali mrefu wa kilometa 10, kwenda Masomoni  kwenye Sekondari ya Kata iliyoko Kijijini Masinono.

Jimbo la Musoma Vijijini lenye Kata 21, lina Sekondari za Kata 26, na 2, za Binafsi. Sekondari mpya 6 zimepagwa kufunguliwa mwaka huu. Matayarisho ya kuanza ujenzi wa sekondari nyingine sita (6) Jimboni humo  yamekamilika.