December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wazazi Urambo watakiwa kulinda afya za watoto wao

Na Allan Kitwe, TimesMajira Online, Urambo

WAZAZI na Walezi Wilayani Urambo Mkoani Tabora wametakiwa kulinda afya za watoto wao kwa kuhakikisha wanawapeleka kliniki ili wakue katika afya njema.

Wito huo umetolewa jana na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa Halima Mamuya alipokuwa akiongea na wakazi wa kata za Kiloleni na Usoke Wilayani humo.

Amesema watoto wakipewa malezi mazuri watakua na afya njema na kuwa msaada mkubwa kwa wazazi, walezi na taifa kwa ujumla.

Amesisitiza kuwa kuporomoka kwa maadili kunavyoshuhudiwa sasa miongoni mwa jamii kunasababishwa na malezi duni ya wazazi jambo linalopelekea kuongezeka kwa watoto wa mitaan.

Mamuya amebainisha kuwa licha ya maboresho makubwa ya huduma za afya baadhi ya akinamama hawapeleki watoto kliniki.

Ameitaka jamii kutambua kuwa mtoto umleavyo ndivyo akuavyo hivyo akaomba wabadilike.

Akizungumzia miradi ya maendeleo Mamuya amewataka wakazi wa kata hizo kutunza miradi inayotekelezwa katika maeneo yao ili idumu na kunufaisha watoto wao.

Amrsisitiza kuwa serikali inatumia fedha nyingi kutekekeza miradi hiyo, hivyo akawataka kujivunia miradi hiyo na kuunga mkono juhudi za serikali kwa kuitunza.

‘Ndugu zangu tunzeni vizuri miradi inayotekelezwa na serikali katika maeneo yenu ili iwasaidie, msikubali mtu yeyote aharibu miundombinu ya miradi hii’, amesema.

Aidha katika kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa watoto na mmomonyoko wa maadili ameitaka jamii kubadili tabia zao na kuthamini watoto wa wenzao kama watoto wao.

Wakiongea kwa nyakati tofauti madiwani wa kata ya Kiloleni, Salum Hamad na Saidi Kazimile wa Usoke wamemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumwaga fedha nyingi katika kata zao ili kufanikisha utekelezaji miradi ya wananchi.

Wameahidi kusimamia ipasavyo fedha zote zinazoletwa na serikali katika kata zao na kuhakikisha miradi husika inakamilika kwa wakati na thamani ya fedha inaonekana katika kila mradi.