Ashura Jumapili TimesMajira Online, ,Biharamulo
Kati ya watu 281 waliohisiwa kuwa na maambukizi ya virusi vya Marburg tangu kutangaza kuwepo kwa ugonjwa huo Januari 20,2025, wawili wamepoteza maisha,huku 145 waliwekwa chini ya uangalizi maalum katika vituo mbalimbali baada ya kusambaa kwa ugonjwa huo katika Wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Afya watu 145 wameruhusiwa kuungana na familia zao,baada ya wataalam wa afya kujiridhisha kuwa hawana maambukizi ya virusi hivyo.
Naibu Waziri wa Afya Dkt.Godwin Mollel, Januari 28,2025, alifanya ziara ya kutembelea kambi za wahisiwa wa virusi vya Marburg katika Wilaya ya Biharamulo na kupata taarifa juu ya mwenendo wa ugonjwa huo kutoka kwa Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara hiyo,Dkt. Ntuli Kapologwe.
Dkt.Mollel,amesema mpaka sasa watu wawili wa familia moja wamepoteza maisha huku wahisiwa 44,wakiendelea kuwekwa chini ya ungalizi wa wataalam wa afya wakiwa nyumbani mwao.
Amesema wahisiwa 92 wanaendelea na uangalizi katika kambi mbalimbali za kutolea huduma za afya kwa kufanya uchunguzi mbalimbali na kujua hali zao zinaendeleaje ndani ya siku 21.
Pia amesema kwa ushirikiano wa Mashirika ya kimataifa na Wahudumu wa Afya ngazi ya jamii tayari Kaya 10,892 wamepatiwa elimu ya kujikinga huku vituo vya ukaguzi wa abiria wanaotoka nchi mbalimbali vikiongezeka kutoka vituo 8 hadi 11,kwa siku abiria 8,000 hadi 10,000 wanapimwa hali zao.
Mollel ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari kwa kufuata sheria zinazotolewa na Wizara ya Afya,ili kuendelea kukinga afya zao bila kuathiri uchumi wao.
Amesema Serikali inaendelea chukua hatua za haraka juu ya masuala ya magonjwa ya milipuko na kuhakikisha familia na jamii za wahisiwa na wote walioko katika kambi wanapata huduma zinazostahili, ili kuwa chini ya uangalizi bila wasiwasi.
“Nawapongeza wataalam wetu kwa kuchukua hatua za haraka mlizofanya na mnaendelea kutoa huduma katika jamii , ugonjwa huu ni hatari na wananchi wanatakiwa kuchukua tahadhari , kwa kuwa hatua za kujikinga ziko wazi basi wanaweza kuendelea na shughuli zao huku wakijikinga,”.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa kinga toka Wizara ya Afya Dkt.Ntuli Kapologwe,ameyataja mashirika ya kimataifa yanayoendelea kutoa huduma huko Biharamulo kuwa ni WHO,UNICEF na CDC ambao wanaendelea kisaidia Serikali katika mapambano ya ugonjwa huo mpaka sasa.
“Serikali yetu kwa kushirikiana na wataalamu wa Afya tumeondoa hofu katika jamii na shughuli zinaendelea kama kawaida huku tukiwa na furaha kuwa hatujapata kesi mpya ya mgonjwa,”amesema Kapologwe.
More Stories
Ilemela yakusanya bilioni 7, mapato ya ndani
Madiwani Ilemela wapitisha rasimu ya bajeti bilioni 84.3
Premium Active Tanzania yapunguza uhaba wa madawati Mlele