December 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wawili wadakwa na polisi tuhuma za kumuua Mwenyekiti UVCCM

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya

WATU wawili wanashikiliwa na jeshi la polisi mkoani Mbeya kwa tuhuma za mauaji ya aliyekuwa Mwenyekiti wa UVCCM Tawi la Machinjoni Kata ya Bwawani wilayani Chunya, Michael Kalinga (36) kwa kumpiga na kitu butu kichwani sehemu ya utosini.

Hata hivyo inaelezwa kuwa mara baada ya mauaji hayo wauwaji hao walifanikiwa kumpora pikipiki marehemu yenye namba za usajili MC.464 ELL aina ya Kinglion.

Akizungumzia tukio hilo Kaimu kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, Wilbert Siwa amesema kuwa tukio hilo limetokea Disemba 2,2024 majira ya saa 5.30 usiku huko Mianzini eneo la Mikoroshini wilaya ya Chunya.

Kamanda Siwa amesema kuwa marehemu alikutwa amefariki dunia na mwili wake kutelekezwa porini umbali wa mita 250 kutoka barabara ya Makongolosi kuelekea Lupatingatinga baada ya kupigwa na kitu butu kichwani sehemu ya utosini na watu ambao hawakufahamika kabla ambao pia walifanikiwa kumpora Pikipiki yenye namba za usajili MC.464 ELL aina ya Kinglion.

Hata hivyo Kamanda Siwa amesema kuwa polisi ilifanya msako mkali Disemba 3, 2024 huko Mlowo Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao ambao wanatuhumiwa kuhusika na tukio hilo wakiwa na Pikipiki waliyopora kutoka kwa Michael Andarson Kalinga (36) na kuwa upelelezi wa shauri hili unaendelea ili hatua nyingine za kisheria zifuate.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa onyo kwa baadhi ya wananchi ambao wanaendelea kujihusisha na vitendo vya uhalifu kuacha mara moja kwani uhalifu haulipi na badala yake wajihusishe na shughuli halali za kujipatia kipato.