December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wawili mbaroni kwa tuhuma za wizi wa pikipiki tatu, za Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Watu wawili akiwemo raia wa Burundi wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Mwanza kwa tuhuma za wizi wa pikipiki tatu mali ya Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema.

Akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbrod Mutafungwa, ameeleza kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 20,2023 muda wa saa tisa usiku huko katika kituo cha afya Mwabaluhi, Kata ya Nyatukara, Wilaya ya Sengerema ambapo wahalifu hao walivunja ofisi ya Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo na kuiba pikipiki hizo zote aina ya Yamaha zenye thamani ya shilingi za kitanzania milioni 11.85 na kuziuza wilayani Kiteranyi, Mkoa wa Mazaganzira nchini Burundi.

Mutafungwa amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Nyokindi Anatory, miaka 44, mkazi wa nchi jirani (Burundi) na Ibrahimu Elisha(55), mkazi wa Ngara mkoani Kagera.

Ambapo ameeleza kuwa watuhumiwa wote wamehojiwa kwa kina na watafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.

Na katika tukio jingine Kamanda huyo wa Polisi ameeleza kuwa jeshi hilo linamshikilia Innocent Juma(35) mkazi wa Kiseke kwa sababu za kiupelelezi kutokana na tuhuma za kujeruhiwa kwa Oriva Ashery(21),mkazi wa Nyasaka, wilayani Ilemela.

Ameeleza kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 22,2023 majira ya saa nane na nusu mchana huko maeneo ya Msumbiji, Kata ya Nyasaka baada ya Innocent Juma kumpigia simu Oriva Ashery na kumtaka afike katika kiwanda cha pipi kiitwacho Jusa kilichopo Nyasaka-Kiloleli na baada ya kufika eneo hilo ghafla alijitokeza mke wa Innocent Juma aitwaye Frazia Celestine na kuanza kumshambulia na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za mwili wake.

“Tunaendelea na jitihada za kumsaka na kumkamata mtuhumiwa aliyetoroka baada ya kutenda kosa hilo la kumjeruhi Oriva Ashery,chanzo cha tukio hilo ni wivu wa kimapenzi ambapo Oriva alipatiwa matibabu katika hospitali ya Mkoa Sekou-Toure na hali yake inaendelea vizuri,”ameeleza Mutafungwa.

Hata hivyo ametoa wito kwa wananchi kuendelea kufichua matukio ya uhalifu na wahalifu katika jamii ili kuweza kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wahalifu pamoja na kuwataka watu wachache ambao bado wanajihusisha na vitendo vya uhalifu waache mara moja kwani hawatosita kuchukua hatua kali za kisheria.