Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online
WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi Prof.Makame Mbarawa amewaalika wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nchi za Norway na Uingereza kuja kuwekeza katika sekta mbalimbali za uchumi na huduma hapa Tanzania hususani kwenye sekta ya ujenzi wa miundombinu.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufungua mkutano uliowaleta pamoja watendaji wa taasisi za Serikali na Ujumbe wa Wawekezaji na wafanyabiashara 37 kutoka nchini za Norway na Uingereza ulioratibiwa na Norwegian-African Business Association na Kampuni ya Invest Africa kwa kushirikiana na Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC), Prof Mbarawa aliwahakishiwa wawekezaji hao kuwepo kwa mazingira mazuri ya uwekezaji na kufanya biashara.
Amesema uwekezaji katika sekta ya miundombinu hususani ujenzi wa barabara na reli itasaidi kufungua fursa lukuki za kibiashara na uwekezaji kwenye nyanja zingine za ki uchumi na kijamii zilizopo hapa nchini.
“Mpaka hivi sasa kwa upande wa mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa wa SGR umefikia asilimia 97 lakini hii inatoa haitoshi kwa kuwa kuna baadhi ya maeneo nchini bado yanahitaji huduma ya reli kwa kuwa ni maeneo yenye shughuli kubwa za uzalishaji”, amesema Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa ameongeza kuwa uboreshaji wa miundombinu haiitaji nguvu ya serikali pekee kwa kuwa serikali inatoa fursa kwa wadau na wawekezaji kuwekeza nchini jambo ambalo limekuwa likifanywa hata na mataifa yaliyoendelea.
“Ninachukua nafasi hii kuwahamasisha muje kwa wingi na serikali yetu sikivu iliyo chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inawathamini wawekezaji hasa kwenye kuwashirikisha kwenye miradi mikubwa ya miundombinu ambayo itakwenda kuifungua nchi kimaendeleo na kutoa fursa kubwa ya ajira nchini”, amesema Prof. Mbarawa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji TIC, Dkt. Maduhu Kazi mbali ya kuwahakikishia ushirikiano mkubwa wafanyabiashara na wawekezaji hao, alibainisha kuwa kituo hicho kitaendelea kutengeneza mazingira mazuri ili kuvutia zaidi na kurahisisha shughuli za uwekezaji nchini.
“Ninapenda kuchukua fursa hii kuwakaribisha sana kuwekeza nchini hasa kwenye maeneo ya fedha, uvuvi, usafirishaji, kilimo na uchukuzi, na niwatoe wasiwasi kwa kuwa serikali imeweka mazingira mazuri zaidi ya uwekezaji”, Amesema Dkt. Maduhu.
Dkt. Maduhu ameongeza kuwa, “Serikali inamatarajio makubwa na nyinyi kuja kuwekeza nchini na hii inadhihirisha kwa kuwa Rais wetu amekuwa mstari wa mbele kuhamasisha uwekezaji na kuitangaza nchini jambo ambalo limepokelewa vizuri na wawekezaji”.
Aidha akizungumza kwa niaba ya Wafanyabiasha na wawekezaji hao, Afisa Mtendaji Mkuu wa Norwegian-African Business Association (NABA) Bw. Eivind Fjeldstad amesema lengo la ujio wao ni kujionea fursa zilizopo nchini na huku akibainisha nia yao ya kuja kuwekekeza kwenye sekta za kilimo, uvuvi, usafirishaji na uchukuzi.
“Hii ni nafasi nzuri kwetu kuwepo hapa, na ni faraja kwetu kuwepo kwenye nchi yenye fursa nyingi ambazo zikitumiwa ipasavyo zitakwenda kuleta tija kwa taifa hili”, amesema, Fjelstad.
Matunda ya ujio ya wawekezaji haya pia yanachangiwa na juhudi kubwa inayofanywa na serikali hasa Rais Samia Suluhu Hassan kwenye kuitangaza nchi na kuvutia wawekezaji mbalimbali kuja kuwekeza jamba ambalo linaangaziwa kuwa lenye kuleta matokeo chanya kwa taifa kwa siku za usoni.
More Stories
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi