November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waweka mkakati maalum utunzaji vyanzo vya maji

Na Martha Fatael, TimesMajira Online

BODI ya Maji bonde la Pangani(PBWB) imeandaa utaratibu maalumu kwa kushirikiana na wadau wa mazingira kupanda miti, kuweka mipaka kwenye vyanzo vya maji Pamoja na mpango wa ufuatiliaji wa miti hiyo mpaka kukua kwake.

Aidha Bodi hiyo imewaonya vikali baadhi ya wananchi wanaojichukulia maji, wanaochimba visima vinavyozidi urefu wa mita 15 bila vibali na wanaofanya shughuli katika mito na vyanzo vya maji ikiwemo upandaji mbogamboga katikati ya mito na mifereji.

Mkurugenzi wa Bodi hiyo, Segule Segule amesema hayo ni sehemu ya maazimio ya kikao cha siku mbili cha jukwaa la kwanza la wadau wa usimamizi wa raslimali za maji katika kidakio cha Kikuletwa kilichofanyika Mjini Moshi.

Segule amesema tayari viongozi na wajumbe wa kikao Cha jukwaa wameotesha miti katika chanzo cha maji Njoro ya Dhobi ambapo pia ikihusisha uoandaji wa miti ya kivuli na matunda.

Amesema maazimio yatawekewa utekelezaji ambapo PBWB itakuwa ikifuatilia na kusaidia kutekeleza maazimio yote ambapo kikao cha mrejesho kitafanyika baada ya miezi sita.

“Naombeni muelewe tumepeana muda wa kutekeleza maazimio haya kuanzia Februari hadi April mwaka huu ili kuanzia Agosti tuandae kikao cha pili kwa ajili ya ufuatiliaji na kuleta mrejesho wa utekelezaji wa haya tuliyokubaliana”amesema.

Amesema maazimio ya kutunga na kusimamia sheria ndogo ndogo za kudhibiti uharibifu na uvamizi katika vyanzo vya maji zinapaswa kusimamiwa na taasisi zote zinazohusika zikiwemo halmashauri.

Awali akichangia katika kikao hicho Mdau Antony Benedict kutoka taasisi ya Kijani Pamoja ambaye pia alichaguliwa rasmi kuwa mwenyekiti wa jukwaa hilo kwa kipindi cha mwaka mmoja, amewataka wadau kuonyesha ushirikiano kukabili hali isiyoridhisha ya upatiakanaji wa maji.

Amesema tasisi hiyo inayozalisha miti kwa ajili ya kutoa bure kupanda maeneo mbalimbali ili kutunza mazingira inautaratibu wa kutoa na kufuatilia utunzaji na ukuaji wa miti hiyo tofauti na hali iliyozoeleka ya kupanda miti na kuiacha ikue bila utaratibu.

Kwa upande wake Mhifadhi mkuu wa Kinapa Betrita Loibok ambaye pia alichaguliwa kuwa makamu mwenyekiti wa jukwaa hilo la Kikuletwa, ametoa rai kwa tasisi zote zinahusika na utunzaji na uhifadhi wa mazingira kuwasiliana hususani kabla ya utoaji wa vibali vyovyote vya matumizi ya raslimali hizo ili kuepuka mgongano.

Kadhalika muhifadhi huyo amewataka wadau wa mazingira kutoona wanyamapori kama wameingilia na kufanya uharibifu katika vyanzo vya maji wakati vyanzo hivyo vipo kwenye maeneo ya hifadhi ya Kinapa kwani hilo ni eneo la Wanyama.

Akifunga kikao hicho Mkuu wa wilaya ya Arumeru, mhandisi Richard Ruyango ameomba wadau wa jukwaa hilo kuweka nguvu ya Pamoja na ushirikiano wa karibu katika utekelezaji wa maazimio Zaidi ya kumi yaliyowekwa na kikao hicho ili kuonyesha thamani ya fedha za kikao hicho.

Mkurugenzi wa Bodi ya majibonde la Pangani, Segule Segule akiongoza zoezi la upandaji miti kabla kufunga kikao cha kwanza cha jukwaa la wadau wa usimamizi wa raslimali za maji katika kidakio Cha Kikuletwa