December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wavuvi 14 wakamatwa Singida

Na Nathaniel Limu, TimesMajira Online, Singida

HALMASHAURI ya manispaa ya Singida,imefanikiwa kukamata wavuvi 14 kwa tuhuma ya kuvua samaki kipindi ambacho maziwa ya Kindai na Singidani yamefungwa.Yamefungwa  kwa shughuli za uvuvi kuanzia januari 31 hadi mei 31 mwaka huu,lengo likiwa  kupisha  samaki kuzaliana.

Pia maziwa hayo ambayo kila mwaka huwa yanafungwa,wanatumia muda huo kuboresha mazingira ya majini,ili yawe rafiki kwa samaki na wavuvi.

Akitoa taarifa hiyo,mkuu wa idara ya mifugo na uvuvi katika manispaa ya Singida,Dk.Adrianus Kelekezi,alisema wavuvi hao waliokamatwa,wametozwa faini ya shilingi 650,000 katika kipindi cha mwezi februali.Pia katika kipindi hicho,wavuvi wamelipia leseni zao mpya, zaidi ya shilingi 620,000.

Amefafanua kwamba wavuvi hao wamekamatwa kwenye operesheni endelevu ambayo itaendelea kukagua maziwa hayo usiku na mchana.

“Tumefanikiwa kutoa elimu juu ya uvuvi bora na stahiki, kwa wafanyabishara 156.Na nawaomba sana wakazi wanaoishi kando kando ya maziwa hayo,wasaidie kutoa au kufichua wavuvi wanaokaidi katazo la
uvuvi ,na  wavuvi haramu,kwa ujumla”,amesisitiza Dk.Kalekezi.

Awali mkurugenzi wa  halmashauri ya manispaa ya Singida, Jeshi Lupembe, ameongeza kwa kusema;

“Samaki wakubwa huishi kwenye kina kirefu cha maji.Kipindi hiki cha masika huwa wanatoka huko chini kwenye  kina kirefu cha maji, na kuja kutaga mayai kwenye kina kifupi.Ili kuwalinda tuna utamaduni wa
kufunga shughuli za uvivu, ili samaki wazaliane bila usumbufu”.

Akifafanua zaidi, amesema  wakati wo wote kuanzia sasa, watakuwa na boti ambayo itatumika mchana na usiku, kukagua uvuvi katika maziwam hayo, kama unazingatia sheria zilizowekwa.

“Pia tumeunda kikosi maalum ambacho kitakuwa kinafanya operation za kushitukiza katika maziwa hayo. Lengo likiwa ni kujiridhisha na uvuvi unaofanywa kama unazingatia taratibu zilizowekwa.Uvuvi kama utafanywa kwa mujibu wa sheria,wavuvi,wakazi wa manispaa na manispaa yenyewe kwa ujumla,pande hizo tatu, zitanufaika”,alisema kaimu mkurugenzi Lupembe.

Katika hatua nyingine, kaimu mkurugenzi huyo ambaye pia ni afisa elimu Sekondari manispaa ya Singida,amewataka wavuvi kutumia kipindi hiki cha kusimama kwa uvuvi, kukata leseni za uvuvi kwa mujibu wa sheria

“Vilevile wakitumie kusajili vyombo vya uvuvi kwa mujibu wa sheria, kuandaa vifaa vya kujikinga na ajali majini ikiwa ni pamoja na maboya ya kuvaa (life jackets). Na kuandaa nyavu halali za uvuvi, ili kuepuka matumizi ya nyavu haramu, pale uvuvi utakaporejea”,alisema.

Kwa mujibu wa Dk. Kalekezi maziwa ya Kindai na Singidani kuna aina kuu mbili za samaki, ambazo ni perege na furu. Kuna wavuvi  150 wanaofanya shughuli za uvuvi katika maziwa hayo.

Naye mvuvi anayevua katika maziwa hayo kwa zaidi ya miaka 70 hadi sasa, Salum Kikikomeko, amesema katika maziwa hayo, hakuna  wavuvi wa uhakika, isipokuwa watu wanaoganga njaa tu.Hivyo elimu inatakiwa ili uvuvi wao uwe wa tija.

Aidha, amemwomba  mkurugenzi au maafisa wengine wa manispaa, kujenga utamaduni wa kukutana na wavuvi mara kwa mara, ili kubadilishana maoni/uzoefu  kwa faida ya Manispaa na wavuvi.

Kaimu mkurugenzi manispaa ya Singida,Jeshi Lupembe,akiwa ofisini kwake akitekeleza majukumu yake ya kila siku.Picha na Nathaniel Limu.