Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online,Mwanza
Wananchi zaidi ya 300 wa Kata ya Buhongwa na Lwanhima Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza Novemba 22,2023 wamelazimika kuvumilia mvua iliyokuwa inanyesha wakati wa mkutano wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbroad Mutafungwa wa kusikiliza kero mbalimbali za kiusalama kutoka kwa wakazi wa Kata hizo mbili.
Mkutano huo umefanyika ikiwa ni mwendelezo wa ziara ya Kamanda wa Mutafungwa kutembelea Kata zote za Mkoa huo kwa lengo la kusikiliza kero za kiusalama na kuzitatua sambamba na kutoa elimu.
“Wakati nakuja hapa kulikuwa na mvua kubwa inanyesha na wakati tunakaribia kufika nilikuwa naongea na OCD kuwa mkutano huu tuuahirishe, lakini kadri muda ilivyokuwa unaendelea nikaona mambo yanakuwa mazuri na watu wanaongezeka pasipo kujali hali ya hewa tuliyoikuta hapa,”amesema Mutafungwa na kuongeza kuwa
“Kitendo hicho kinaonesha ni kwa jinsi gani Jeshi la Polisi tunafanya kazi kwa karibu na wananchi wa Kata hii,”.
Kupitia taarifa ya hali ya usalama katika Kata hizo mbili iliyosomwa na Polisi Kata wa Kata ya Buhongwa Mkaguzi Msaidizi wa Polisi (A/Insp) Clement Masululi amesema Kata hizo zina idadi kubwa ya watu ambao ni wakazi na wafanyabiashara.
Hivyo ameomba kuongezewa gari moja kwa ajili ya doria maeneo hayo kwani penye idadi kubwa ya watu na uhalifu pia huongezeka.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Ofisa Polisi Jamii Mkoa Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Denis Kunyanja pamoja na kutoa elimu, pia aliwapongeza wananchi kwa usikivu na uvumilivu wao.
“Kimsingi tuko hapa kwa ajili ya kuzungumzia mambo ya usalama tu, kama mnavyojua usalama ndiyo mtaji namba moja kabla hujafikiria kufanya jambo lolote lazima ufikirie suala la usalama kwanza,”amesema SSP Kuyanja.
Kwa upande wake, Abdulmajid Fadhil mkazi wa Buhongwa ameeleza kuwa eneo hilo kuna upenyezo wa dawa za kulevya kwa siri.
“Zimekuwa zikiingizwa hapa ikiwemo bangi, ambapo vijana wanatumia na kupelekea kuharibu vichwa vyao na kuanza kufanya uhalifu,”.
Aidha Kamanda Mutafungwa ametangaza kuanza kwa operesheni kali dhidi ya wahalifu wanaojihusisha na madanguro, dawa za kulevya na makosa mengine ambayo ni kero kwa jamii pamoja na kuchukua hatua kali za kisheria.
“Ofisa upo hapa, mara baada ya kubandua mguu wetu Operesheni hiyo ianze, vijiwe vyote vya uhalifu vifumuliwe, ili kuhakikisha kwamba vibaka popote walipo wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria,”amesema Mutafungwa.
More Stories
Mwinyi: Kuna ongezeko la wawekezaji Zanzibar
Othman awakabidhi jezi Zanzibar Heroes
Maofisa Watendaji watakiwa kufanya kazi kwa weledi