Na. Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya
WAUMINI wa dini ya Kiislamu wamemuombea dua ya kheri Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini na Spika wa Bunge ambaye pia Rais Umoja wa Mabunge Duniani ,Dkt.Tulia Ackson ili aweze kutekeleza majukumu yake vizuri katika kuhudumia jamii.
Ambapo Abdalah Yundu Shekhe Mkuu wa Wilaya ya Mbeya ameongoza dua ya kumuombea Dkt Tulia Ackson katika kazi zake za kila siku.
Dua hiyo imefanyika Machi 29,2024 wakati Shekhe Ibrahim Bombo akipokea msaada wa vyombo vya kuhubiria msikitini kwa niaba ya Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Mbeya kutoka Taasisi ya Tulia Trust inayoongozwa na Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Dkt.Tulia Ackson katika Msikiti wa Masjid Bi.Fatma iliyopo Nzovwe Jijini Mbeya.
Shekhe Bombo amesema kuwa vyombo vilivyotolewa katika msikiti huo ni vema vikatunzwa kwa uangalifu ili viendelee kutumika katika kuendesha ibada.
Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo kwa niaba ya Dkt. Tulia Ackson Ofisa Habari na Mawasiliano wa Taasisi hiyo, Joshua Mwakanolo amesema lengo ni kutekeleza ombi la msikiti huo kwa Mbunge ambapo waliomba vipaza sauti kwa ajili ya ibada.
Mmoja wa waumini wa Msikiti huo , Hemed Kipengele amesema kitendo kilichofanywa na Dkt. Tulia ni ibada tosha katika kutoa vifaa hivyo kwani hajajali itikadi za kidini.
Kwa upande wake Justin Kayuni ambaye ni Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Ndanyela Kata ya Nzovwe ameipongeza Taasisi ya Tulia Trust kwa kutoa vifaa hivyo kwani vitasaidia kueneza neno la Mungu.
Katika kuhakikisha anafikia jamii bila kubagua Dkt.Tulia amekuwa akitoa misaada mbalimbali bila kujali itikadi za Kidini na kisiasa ambapo hivi karibuni amefanikisha ujenzi wa Misikiti ya Tukuyu Mjini,Kiwira Wilayani Rungwe na Uyole jijini Mbeya
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba