April 15, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waumini Kanisa la KKAM waipeleka Mahakamani bodi ya wadhamini KKKT

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya

SHAURI la maombi namba 1941/2025 la Waumini wa Kanisa la Kilutheri Afrika Mashariki(KKAM) dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT)limesikilzwa mbele ya Jaji Mussa Pomo wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya ambapo KKAM inawakilishwa na Wakili William Mashoke na KKKT ikiwakilishwa na Wakili Peter Kilanga.

Awali Wakili William Mashoke amesema Mchungaji Maka Mwakyusa anawakilisha Waumini kumi na moja ambao ni Astin Mwabusenge, Zackaria Mwafubela,Itika Ngosi,Lwimiko Mwaipopo,Astanton Mwamalumbili,Danford Mwamatepela,Ambakisye Mwankili,Yohana Mwambungu,Paul Mwaituka na Appointment Mwalubilo.

Aidha ameiambia Mahakama kuwa Yohana Mwambungu kuwa anaumwa ilhali Benjamin Mwaisumo hakuwepo mahakamani kwa kile kilichodaiwa kukosa Wakili wa kumuwakisha katika shauri hilo.

Wakili Mashoke amedai shauri hilo  limekuja kwa maombi kabla ya muda kifungu XXXVII 5 mwenendo wa jinai sura ya 33 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Aidha amesema kifungu kidogo cha 44(1na2) sura ya 216/2019 ambapo Wakili William Mashoke ameiomba Mahakama kufanya marekebisho au kumuondoa Benjamin Mwaisumo ambaye hakuwepo mahakamani ili waleta maombi wengine waendelee kweye shauri hilo.

Wazo hilo lilipingwa na Jaji Mussa Pomo akidai mleta maombi anayo haki ya kusikilizwa na shauri hilo pia lilisikilizwa na Msajiri wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya ambaye aliona lisikilizwe na Jaji.

Hata hivyo Jaji Mussa Pomo alipomuuliza Wakili Peter Kilanga aliomba shauri liondolewe Mahakamani kwa kuwa halikukidhi vigezo.

Kwa upande wa Wakili William Mashoke ameiomba Mahakama kuliondoa shauri hilo bila gharama na Wakili Peter Kilanga aliomba shauri hilo liondolewe Mahakamani kwa gharama.

Baada ya kuzisikiliza pande zote Jaji Mussa Pomo alikubali kuliondoa shauri hilo Mahakamani bila gharama kwa kuwa Mahakama ndiyo imeibua hoja za msingi na mjibu maombi hakuwa amewasilisha mapingamizi yoyote mahakamani.

Jaji Mussa Pomo aliliondoa shauri hilo Mahakamani na kuamuru kila upande ubebe gharama zake.

Mgogoro huo umefikishwa mahakamani kila upande ukidai uhalali wa kumiliki Makanisa na mali baada ya baadhi ya waumini kutoka KKKT  kujiunga KKAM.