March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watumushi Wizara ya Nishati wapatiwa elimu ya matumizi ya majiko janja ya umeme

📌 Ni baada ya Dkt.Biteko kuwakabidhi majiko yanayotumia umeme kidogo kwa gharama nafuu

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

Watumishi wa Wizara ya Nishati wamepata elimu ya matumizi bora na sahihi ya majiko yanayotumia umeme kidogo ( Induction cookers), baada ya kukabidhiwa majiko hayo na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko hivi karibuni.

Ambapo Dkt. Biteko aliwakabidhi majiko hayo watumishi wa Wizara ya Nishati ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia pamoja na kwa kutambua ni mabalozi wa utoaji wa elimu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wananchi.

Mafunzo hayo yamefanyika leo katika Ofisi za Wizara ya Nishati- Mtumba mkoani Dodoma yameandaliwa na Kitengo cha Nishati safi ya kupikia kwa kushirikiana na wataalam kutoka kampuni ya Positive Cooker.

Akitoa elimu ya matumizi bora na sahihi ya majiko hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Positive Cooker,Atukuzwe Willson,ameeleza kuwa lengo la utoaji wa mafunzo hayo ni sehemu ya uhamasishaji wananchi kutumia majiko janja yanayotumia umeme kidogo kupikia.
.
“Lengo la kutoa elimu hii ni kuhakikisha kila Mtanzania anaachana na matumizi ya nishati isiyo safi,ili kulinda mazingira pamoja na afya zetu.Pia ni sehemu ya jitihada za kuunga mkono kampeni ya nishati safi ya kupikia ambapo hadi kufikia mwaka 2034 asilimia 80 ya watanzania wanapaswa kutumia nishati safi ya kupikia,”amesema Willson.

Amesema,majiko hayo janja ya umeme yanatumia wastani wa nusu uniti hadi uniti moja na nusu kwa wastani wa dakika 15 mpaka dakika 90 sawa na shilingi 65 mpaka shilingi 534 tu, hali inayothibitisha ufanisi wa majiko hayo kuwa na gharama nafuu, kuokoa muda, kulinda afya pamoja na mazingira.