Na Tiganya Vicent,TimesMajira Online,Tabora
WATUMISHI watatu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hamiku Mkazi wa Mkoa wa Tabora wakituhumiwa za kufanya makosa matatu ya kula njama, kufanya udanganyifu na kutoa taarifa za uongo.
Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Tabora Thomas Milanzi waliosomewa mashitaka hayo ni Hamza Khamis, Sailisi Mbungu na Lekwa Zakayo.
Upande wa mashitaka ukiongozwa na Wakili Tumaini Pius uliiambia Mahakama hiyo kuwa watuhumiwa walitenda makosa hayo kati ya April 08 na 18 /2019 kati ya Kituo kidogo cha Reli cha Igusule na Sonjo.
Wakili Pius alidai katika shitaka la kwanza kuwa April 08/2019 watuhumiwa wakiwa ni watuhumishi wa Shirika la Reli walikula njama kuiba mafuta katika Treni namba X631 iliyokuwa na Injini namba 9017 ikitokea Isaka kuelekea Tabora.
Akisoma Shitaka la pili dhidi ya watuhumiwa wote Wakili Pius alidai kwamba siku hiyo kwa udanganyifu walichukua mafuta aina ya Diesel lita 240 zenye thamani ya shilingi 534,440/= toka kwenye injini ya treni hiyo.
Ilidaiwa katika shitaka la tatu ambalo linamkabili mshitakiwa wa kwanza Hamza Khamis kwamba April 18/2019 akiwa Dereva wa Treni hiyo alitoa taarifa za uongo kwamba lita 1800 za mafuta aliyopewa amezitumia kutoka Isaka Hadi Tabora huku akijua ni uongo.
Watuhumiwa wote walikana mashitaka hayo na wapo nje kwa dhamana hadi Desemba 16 mwaka huu shauri hilo litakapotajwa kwani upelelezi wake bado haujakamilika.
Wakati huo huo watu watatu waliokuwa wanakabiliwa na kesi tofauti za mauaji wamerudishwa rumande baada ya kusomewa maelezo ya awali na kuyakana mbele ya Hakimu Mkazi aliyekasimiwa Mamlaka ya kusikiliza kesi za Mahakama Kuu Jovin Kato.
Washitakiwa hao ni Ramadahani Juma anayeshitakiwa kwa kumuua Said Aman kwa kumchoma kisu shingoni, Shija Mabala anayetuhumiwa kumuua Tua Kishiwa huko Nzega na kwenda kumtupa porini na Athuman Hamis anayetuhumiwa kumuua Rahel Daud kwa kumtenganisha kichwa na kiwiliwili.
More Stories
Kapinga asema mafanikio katika sekta ya nishati yanatokana na jitihada za Rais Samia
Bumbuli kutekeleza miradi kwa kuangalia vipaumbele
Makalla:Kupanga fujo ni dalili za kushindwa uchaguzi