January 12, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watumishi wanaodaiwa kodi ya ardhi kunyang’anywa viwanja

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online,Arusha

NAIBU Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt.Angeline Mabula amewataka watumishi wa sekta ya ardhi katika mkoa wa Arusha wanaodaiwa kodi ya pango la ardhi kuhakikisha wanalipa kodi hiyo vinginevyo watanyang’anywa viwanja wanavyomiliki kama inavyofanyika kwa wananchi wasio watumishi.

Akizungumza hivi karibuni mkoani Arusha na Watendaji wa sekta ya ardhi katika mkoa huo akiwa katika ziara ya kukagua utendaji kazi wa sekta ardhi, Dkt Mabula amewataka wakurugenzi wa Halmashauri za mkoa wa Arusha kuandaa orodha ya watumishi wanaodaiwa kodi ya ardhi na kumpatia ili aweze kuwafuatilia.

Amesisitiza kuwa kwa wale watumishi watakaoshindwa kulipa kiasi wanachodaiwa watanyang’anywa viwanja vyao.

“Wakurugenzi, watumishi wenye viwanja na ambao hawajalipa kodi ya pango la ardhi nataka nipate orodha yao na watakatwa kwenye mishahara yao maana ni deni kama yalivyo madeni mengine, kama huwezi kulipa kubali tuchukue kiwanja chetu au ukubali tuchukue pesa yetu,” amesema Dkt. Mabula.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara yake katika ufuatiliaji wadaiwa sugu wa kodi ya ardhi haiangalii mMashirika, taasisi, makampuni au watu binafsi pekee, bali inaangalia pia watumishi wa umma aliowaeleza kuwa wakati wakichukua viwanja walifahamu kuwa wanapaswa kulipa kodi ya pango la ardhi.

Amegeukia suala la Taasisi za Umma zenye madeni makubwa ya kodi ya pango la ardhi, Dkt Mabula alisema mpango wa kulipa madeni hayo kwa taasisi hizo umeshawekwa ikiwemo kuwasiliana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali namna ya kuzibana taasisi za umma na kusisitiza kuwa kwa zile ambazo zimeonesha nia ya kulipa ziendelee kukamilisha madeni yao ili kuepukana na mkondo wa sheria.