Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka watumishi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani Kilolo kulitunza jengo jipya la ofisi pamoja na miundombinu yake ili litumike kikamilifu katika kuzuia na kupambana na rushwa kama ambavyo Serikali ya Awamu ya Sita imekusudia.
Ndejembi ametoa maelekezo hayo kwa watumishi wa TAKUKURU wilayani Kilolo, wakati akikagua ujenzi wa jengo jipya la TAKUKURU linalojengwa katika halmashauri hiyo kwa lengo la kuwawekea mazingira rafiki yatakayowawezesha kutekeleza ipasavyo jukumu la kuzuia na kupambana na vitendo vya rushwa.
“Ninawaasa mtakaokuwa mnatumia ofisi hii, muitunze ofisi na miundombinu yake na wala msiwasubiri viongozi wa ngazi za juu kutoka makao makuu ya TAKUKURU waje kuwaelekeza namna ya kuitunza kwani jukumu la kuitunza ni lenu,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.
Mhe. Ndejembi ameongeza kuwa, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamishna wa Polisi, Salum Hamduni amekuwa mstari wa mbele kupigania maslahi ya watumishi wa TAKUKURU hivyo ni jukumu la watumishi hao wa TAKUKURU wilayani kilolo kuunga mkono jitihada za kiongozi wao kwa kuitunza ofisi hiyo mpya na miundombinu yake ili iwe na tija katika kuendeleza mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa kwenye wilaya hiyo.
Aidha, Mhe. Ndejembi ameushukuru uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo kwa kuwapatia TAKUKURU eneo la kujenga ofisi ambayo kwa kiasi kikubwa, itasaidia kuongeza ufanisi wa watumishi wa TAKUKURU kiutendaji.
Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bi. Neema Mwakalyelye ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha ujenzi wa jengo hilo litakaloimarisha utekelezaji wa jukumu la kuzuia na kupambana na vitendo vya rushwa wilayani Kilolo.
Ameongeza kuwa, ujenzi wa jengo hilo utasaidia kuweka mazingira rafiki kwa wananchi wa Kilolo kupata huduma za jamii kwa wakati, bila kuombwa au kutoa rushwa.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amefanya ukaguzi wa jengo jipya la TAKUKURU wilayani Kilolo ili kujiridhisha na maendeleo ya ujenzi huo.
More Stories
ITA chatakiwa kutoa mafunzo ya viwango vya juu na kasi ya maendeleo ya Kisayansi
Wagombea CHADEMA wakipewa ridhaa,watakuwa wawazi
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake