November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watumishi wa e-GA wahimizwa kufanya kazi kwa kuzingatia misingi mikuu sita ya Mamlaka

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Dar es Salaam.

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), Mhandisi Benedict Ndomba, amewataka watumishi wa Mamlaka hiyo kufanya kazi kwa kuzingatia misingi mikuu sita ya Taasisi.

Ndomba amesema hayo wakati wa kikao cha Watumishi wa Mamlaka kilichofanyika kwakipindi cha siku tatu katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuwajengea uwezo watumishi hao katika masuala mbalimbali yanayohusu utumishi wa umma

“e-GA inaongozwa na misingi mikuu sita ambayo inaelekeza kuhusu tabia na mwenendo wa watumishi wake kwa ngazi zote na kufafanua utamaduni wa mahali pa kazi ili kuhakikisha watumishi wote na wateja wa Mamlaka, wanao uelewa wa pamoja wa jinsi wanavyotakiwa kuhudumiwa na nini kichotarajiwa kutoka kwao,”amesema Ndomba.

Aidha, Ndomba amewakumbusha watumishi wote wa Mamlaka kuzingatia misingi hiyo ambayo ni uadilifu, ubunifu, kutathmini wateja, ushirikiano, kufanya kazi kwa pamoja na weledi katika utendaji kazi wao wa kila siku.

Amefafanua kuwa, Mamlaka imekuwa taasisi ya mfano inayofanya shughuli zake za kila siku kwa kasi na ari inayokubalika, kutokana na uadilifu mkubwa wa Menejimenti na watumishi waliodhamiria kuweka juhudi kubwa katika kuboresha utendaji wa Serikali na utoaji huduma bora kwa umma.

“Nawakumbusha watumishi wote kuimarisha uadilifu na kila mtumishi kutimiza wajibu wake kwa kufanya kazi kwa bidii, nidhamu na kwa weledi kwa kuzingatia misingi hiyo huku Mamlaka ikiendelea na jitihada mbalimbali za kuhakikisha kuwa watumishi wanafanya kazi katika mazingira bora na salama”,amesisitiza Ndomba.

Katika kikao hicho mada mbalimbali zilizolenga kujenga uelewa na ufahamu kwa watumishi ziliwasilishwa ikiwemo Afya mahali pa kazi, Rushwa mahala pa kazi, Maadili ya utendaji, Haki na Wajibu, HIV/AIDS na magonjwa sugu yasiyoambukiza, mawasiliano mazuri kwa utendaji bora wa kazi, Namna ya kukabiliana na msongo wa mawazo na maisha kazini.

Aidha, Kikao hicho kilihitimishwa na Bonanza la Michezo lilifanyika katika viwanja vya gymkhana michezo mbalimbali ikiwemo kukimbiza kuku, kuvuta kamba, kutembea kwa kutumia magunia, kutembea na yai kwenye kijiko, mbio fupi.