Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online
Watumishi wa Bodi ya Mfuko wa Barabara wametakiwa kuzingatia miongozo ya nyaraka mbalimbali za kiserikali ili kuboresha ubora na ufanisi wa mawasiliano ya kimaandishi ndani ya Serikali.
Hayo yamesemwa Aprili 16, 2025 na Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa Wizara ya Ujenzi,Mrisho Mrisho, wakati wa kufunga kikao cha ndani cha Bodi ya Mfuko wa Barabara kilichofanyika mkoani Morogoro.

Mrisho ameeleza kuwa miongozo hiyo inaweka viwango vya uandishi wa nyaraka kama barua rasmi, ikiwa na lengo la kuweka muundo wa pamoja katika mawasiliano ya kiserikali.
Aidha, amewataka watumishi wa Bodi hiyo kuboresha mahusiano na mawasiliano ya ndani ili kuongeza tija na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Bodi hiyo, Rashid Kalimbaga, amesema jumla ya watumishi 32 wameshiriki katika kikao hicho kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kitaaluma na kiutendaji.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Mipango na Mapato, Godlove Stephen, ameahidi kuwa mafunzo hayo yatatumika kuboresha uandishi wa taarifa mbalimbali za Bodi na kuimarisha ushirikiano miongoni mwa watumishi.
Mtumishi wa Bodi, Afia Ndyamukama, ametoa rai mafunzo kama hayo yawe endelevu ili kuimarisha uwezo wa watumishi katika mazingira ya kazi.

More Stories
Chalamila:Dar ni salama,aelezea mafanikio na mipango ya maendeleo ya Mkoa
Ulaji vyakula vya aina moja,umri vyatajwa ongozeko la matatizo ya macho Mbeya
Kenya,Uganda zaanzisha mradi wa uendelezaji rasilimali za maji Angololo