January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watuhumiwa watano, mashine za boti za uvuvi mbaroni

Na Ashura Jumapili ,TimesMajira online Kagera,

Jeshi la Polisi Mkoa wa Kagera limefanikiwa kukamata mashine 12 za boti za kuvua samaki na pikipiki,zilizoibiwa ndani ya Ziwa Victoria mkoani humo.

Akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake Kamanda wa Polisi Mkoa wa kagera ,Blasius Chatanda,amesema katika tukio hilo, wamefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wa tano wa wizi na wanunuzi ambao majina yao hayakutajwa kwa sababu za kiuchunguzi na kudai kuwa zoezi hilo ni endelevu.

Amesema,ukamataji wa mashine hizo umefanikiwa kupitia msako, ulioanza mwishoni mwa Juni hadi Agosti 12 mwaka huu,iliyoanzia ziwani baada ya kupata taarifa ya uwepo wa wizi wa mashine hizo.

Chatanda,amesema mashine hizo kutoka kampuni tofauti zilikamatwa Wilaya ya Bunda na Musoma mkoani Mara,Bariadi na Busega.

“Tunaamini hakuna wizi wa mali kama hakuna mnunuzi, hivyo tumezingatia pande zote mbili kuwakamata ili kukomesha wizi huo,”amesema kamanda huyo.

Jeshi la polisi linatoa wito kwa watu walioibiwa mashine zao wafike kituo cha Polisi Bukoba kuzitambua maana wengine walikuwa wameanza kubadilisha muonekano wa awali wa mashine hizo

Katika hatua nyingine amesema wamefanikiwa kukamata pikipiki 6 kutoka kampuni tofauti na kuwataka waliopoteza pikipiki zao kufika kuzitambua.

Hata hivyo aliwataadhalisha wanaotegemea kuiba kubadili mfumo wao wa maisha kwa sababu Mkoa wa Kagera sio sehemu sahihi kwa matukio ya uhalifu hasa wizi.

Aidha,amewashukuru wananchi waliotoa taarifa za uhalifu huo kwa jeshi la polisi mapema na kufanikiwa kuzikamata na kuwataka waendelee kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo ili wahalifu waweze kudhibitiwa haraka.