December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watuhumiwa wa wizi wa vifaa ujenzi wa SGR Isaka-Mwanza mbaroni

Judith Ferdinand, TimesmajiraOnline,Mwanza

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limefanikiwa kukamata lita 4,426 za mafuta ya aina mbalimbali ikiwemo Dissel na Petrol, pia linawashikilia watu 9 kwa tuhuma za makosa mbalimbali ikiwemo wizi wa vifaa katika mradi wa reli ya kisasa SGR.

Akizungumza Jijini hapa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza SACP- Wilbroad Mutafungwa ameeleza kuwa operesheni hiyo iliyoanza Januari 11,2023 katika maeneo ya vijiji vya Isunga, Nkalalo-Bukwimba, Malya na Usagara wilayani Kwimba na Misungwi.

Ambapo imefanikiwa kukamata mifuko ya saruji 646 aina ya Huaxin na bomba 28 za vyuma zinazodhaniwa kuwa mali za mradi wa Serikali wa SGR unaojengwa toka Isaka mkoani Shinyanga hadi Mwanza.

Ameeleza kuwa pikipiki tatu zimekamatwa moja aina ya SUN LG yenye namba MC 507 BCY, ya pili ni aina ya KING LION yenye namba MC 199 DMN na ya mwisho ni aina ya KING LION ambayo plate namba yake imekutwa imetolewa na watuhumiwa hao kwa lengo la kutofahamika wakati wakitekeleza uhalifu.

Pia amewataja watuhumiwa waliokamatwa kuwa ni Luyola James , miaka 34, msukuma, mfanaybiashara, mkazi wa kijiji cha Isunga
Specioza Samsoni, miaka 22, mkazi wa kijiji cha Isunga.

Huku wengine ni Deshi Katwale, miaka 42, mkazi wa Nkalalo,Mathias Magadulla @ Bulengela, miaka 47, mkazi wa Nkalalo
Salimu Nassoro, mkazi wa Malya, Mfanya biashara na Michael Juma Bigazi, miaka 35, mkazi wa Usagara.

Aidha Mutafungwa ameeleza kuwa msako mkali bado unaendelea maeneo hayo wa kukamata mtandao wa watu wote wanaohujumu mradi huo mkubwa wa Serikali unaogharimu mabilioni ya fedha.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linaendelea kuwaomba wananchi kutoa ushirikiano ili kuweza kudhibiti wezi hao wenye malengo ya kurudisha nyuma maendeleo ya Taifa letu.

Katika tukio jingine Kamanda huyo ameeleza kuwa ni la wizi wa pikipiki Wilaya ya Magu lililotokea Januari 14,2023 muda wa saa 3 (21:00) usiku, katika kitongoji cha Mwanduru, kata ya Bujora, tarafa ya Sanjo.

Ambapo kuliripotiwa taarifa kuwa kuna mwananchi aitwaye Omary Shabani, miaka 20, Dereva bodaboda na mkazi wa kijiji cha Mwamanyiri, amevamiwa na kuporwa pikipiki yake aina ya Tvs yenye namba za usajili MC 450 DLM rangi nyeusi.

Jeshi la Polisi lilianza ufuatiliaji wa haraka juu ya taarifa hiyo na ilipofika Januari 15 muda wa saa sita na dakika 30 (00:30) usiku katika eneo la Busisi wilaya ya Misungwi lilifanikiwa kuwakamata watuhumiwa watatu wakiwa na pikipiki hiyo iliyotambuliwa kuwa mali ya Omary Shabani na ndiyo iliyoibiwa Kisesa wilayani Magu.

Ameeleza kuwa watuhumiwa wa wizi wa pikipiki waliokamatwa ni Michael Silyvester, miaka 36, mkazi wa Kisesa,Evarist Masumbuko, miaka 24, mkazi wa Kisesa isesa na Bahati Charles, mkazi wa Sengerema.

Watuhumiwa wanaendelea kuhojiwa kwa kina na upelelezi wa shauri hili unakamilishwa haraka iwezekanavyo na watafikishwa kwenye vyombo vya sheria.