October 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha

Watuhumiwa wa kilo 1,200 za bangi Arusha kortini

Na Grace Gurisha, TimesMajira Online

WAKULIMA wawili wakazi wa Mwandeti jijini Arusha, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka ya kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya aina ya bangi yenye uzito wa zaidi ya kilo 1,200.

Washtakiwa hao Seuli Mollel na Losieku Mollel, walifikishwa jana mahakamani hapo na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya.

Katika hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo na wakili wa Serikali mbele ya Hakimu Mkazi, Gwantwa Mwankuga alidai watuhumiwa hao wanashtakiwa chini ya kifungu cha sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya sura ya 95 ya sheria za Tanzania.

Inadaiwa kuwa, Juni 2020 katika Kijiji cha Longilong wilayani Arumeru mkoani Arusha, mshtakiwa Seuli alikutwa na kilo 649.5 za dawa ya kulevya aina ya bangi huku mshtakiwa Losieku akikutwa na kilo 728.9 za dawa hizo za kulevya.

Washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka kisheria kusikiliza kesi za uhujumu uchumi ambazo husikilizwa Mahakama Kuu au mahakama za chini kwa kupatiwa kibali kutoka kwa DPP.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai 22, 2020 itakapokuja kwa ajili ya kutajwa, watuhumiwa wamerudishwa rumande.