January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watu wenye ulemavu waomba serikali kupeleka mahitaji yao kuanzia ngazi ya zahanati

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya

WATU wenye Ulemavu jijini Mbeya wameitaka Serikali kupeleka mahitaji yao kuanzia katika ngazi ya Zahanati pindi wanapopata changamoto mbalimbali na kuweza kutibiwa kama wagonjwa wengine ili kuepuka usumbufu wa kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za matibabu.

Aidha wamesema ili jambo hilo liweze kuwa na msisitizo kwa watoa huduma za afya ni vema maelekezo hayo yakatambulika kwenye katiba hali itakayopelekea kila mwenye dhamana kutekeleza kwa vitendo na ulazima kutokana na matakwa ya kikatiba.

Walitoa maoni hayo Julai,27 ,2024 wakati wa kongamano la Katiba lililoandaliwa na Jukwaa la Katiba nchini lililofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya GR City uliopo jijini hapa lililowakutanisha watu wenye mahitaji maalum, boda boda, mama ntilie, wauza mbogamboga, madereva wa bajaji na Vijana.

Nemes Temba Mwenye ulemavu wa ngozi amesema mahitaji ya watu wenye ulemavu yakiingizwa kwenye katiba itakuwa rahisi wao kupata matibabu kuanzia ngazi ya chini jambo ambalo litawaondolea changamoto ambazo wanakumbana nazo kwa sasa.

“Katiba mpya ioneshe wazi mahitaji ya wenye ulemavu ili wahusika waweze kubanwa na kuwajibishwa pindi wanapokosa kutekeleza jambo hilo kwani katiba ya sasa haielezi chochote kuhusu sisi hivyo hata tukihitaji haki zetu hatuna sehemu ya kukimbilia” amesema Temba ambaye ni Mwalimu wa Shule ya wenye mahitaji maalum ya Child Support Tanzania.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Dkt. Ananilea Nkya amesema ni vema katiba mpya ielekeze masuala ya wenye ulemavu maana iliyopo haisemi chochote ikiwa pia ni pamoja na kuelekeza kila makazi yanayojengwa mitaani kuzingatia mahitaji ya walemavu.

Naye Damas Mwambeje amesema pia Katiba mpya inapaswa kutoa msamaha wa bei ya vifaa vya utengamavu ili vipatikane kwa gharama nafuu ili kila mwenye uhitaji aweze kupata kirahisi ikiwa ni pamoja na kusisitiza vifaa hivyo kupatikana katika ngazi za chini ikiwemo zahanati.