January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online, Mwanza 

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limefanikiwa kudhibiti jaribio la uhalifu,lililotokea, Januari 9,2025, majira ya saa mbili na dakika 45 usiku(20:45 hrs), mtaa wa Kabambo Kata ya Kiseke, wilayani Ilemela mkoani Mwanza.

Akizungumza  Januari 10,2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbroad Mutafungwa, amesema watu wawili wa jinsi ya kiume wanaodhiniwa kuwa ni majambazi,waliokuwa wamevaa mavazi ya kike ambayo ni gauni na vilemba,kwa lengo la kuficha jinsi na muonekano wao ambao majina na anuani zao hazikuweza kufahamika,waliuawa kwa kupigwa risasi na Askari polisi waliokuwa wakifanya doria maeneo hayo.

Tukio hilo lilitokea baada ya watu hao kuvamia nyumbani kwa mfanyabiashara aitwaye Flora Sungura Abdallah,(42), mkazi wa mtaa wa Kabambo.Ambapo watuabhso wanaosadikiwa kuwa ni majambazi walivamia nyumba hiyo kwa lengo la kufanya uhalifu na walifanikiwa kuingia ndani wakati mfanyabiashara huyo alipofunguliwa geti akitoka kwenye shughuli zake za kibiashara. 

Mutafungwa amesema,watu hao walikuwa na bunduki aina ya Shortgun moja iliyotengenezwa kienyeji ikiwa na risasi mbili na mapanga mawili,ambapo  wakazi wa eneo hilo waliweza kupiga kelele za kuomba msaada na taarifa hizo kufika kwa askari polisi waliokuwa doria katika eneo hilo. 

“Askari wa Jeshi la polisi kwa haraka walifika eneo la tukio kwa ajili ya kutoa msaada na kuwataka watu hao kujisalimisha  mara moja, watu hao wenye silaha walikaidi amri ya Askari na kutaka kuwadhuru wakazi wa nyumba hiyo pamoja na askari wetu. Ndipo askari walifyatua risasi na kusababisha watu wawili ambao mmoja alishika bunduki na mwingine akiwa na panga kujeruhiwa kisha kupoteza maisha papo hapo,” amesema Mutafungwa.

Pia amesema,miili ya watu hao ambayo hata hivyo haijatambuliwa imehifadhiwa katika hospital ya Rufaa Bugando ikisubiri utaratibu wa utambuzi na uchunguzi wa kitaalamu (Post mortem),katika tukio hilo hakuna mali iliyoibiwa. 

“Katika tukio hilo silaha aina ya Shortgun moja, mapanga mawili na begi la mgongoni likiwa na nguo suruali, shati, bisibisi na viatu vimepatikana kwenye eneo la tukio,huku watu  wawili wa jinsia ya kiume ambao walikuwa ni washiriki katika tukio hilo hawajafahamika majina na sura walifanikiwa kutoroka kwa kutumia usafiri wa pikipiki ambayo namba za usajiri hazijafahamika,”amesema  Mutafungwa na kuongeza:

“Msako wa kuwatafuta watu hao waliokimbia na watu wengine ambao walipanga na kuratibu tukio hilo la kihalifu unaendelea, ili waweze kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria,chanzo cha tukio hili ni kujipatia mali kwa njia isiyo halali,”.

Sanjari na hayo ametoa onyo kwa  baadhi ya watu wanaopenda kutafuta ridhiki kwa kufanya vitendo vya kihalifu yakiwemo matukio ya ujambazi, uvunjaji na matukio mengine, hivyo wanapaswa kutambua kuwa Mkoa wa Mwanza siyo sehemu ya kufanyia matukio hayo.Hivyo jeshi hilo  limejipanga kuendelea kuwasaka wahalifu wote popote walipo na kuwakamata ili waweze kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria. 

“Tunaomba wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kuwafichua wahalifu na uhalifu huku tukiwakumbusha wafanyabiashara kuweka CCTV Camera katika maeneo yao ya biashara na nyumbani ili kurahisisha jitihada za polisi za kuwabaini na kuwadhibiti wahalifu,”.