May 18, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watu wanne mbaroni kwa tuhuma za wizi wa vifaa vya mradi Miji 28

Na Esther Macha Timesmajira Online, Mbeya

WATU wanne wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Mbeya kwa tuhuma za wizi wa vifaa vya mradi wa kimkakati wa maji wa Miji 28,kwa wizi wa mabomba 50, ya chuma na “levelling mashine” pamoja na stendi yake ambavyo hutumika kwenye ujenzi wa mradi huo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi,Benjamini Kuzaga, amesema kuwa tukio hilo limetokea Aprili 22 na Mei 15,2025 wakati wa misako inayoendelea katika maeneo mbalimbali jijini humo.

Kuzaga amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Edwin Liweuli, Chesco Muheze mlinzi wa mradi, Hamza Madete wote wakazi wa Igawa wilayani Mbarali na Victor Timbulo mkazi wa Ifakara mkoani Morogoro.

Amesema watuhumiwa hao waliiba vifaa hivyo kwa kushirikiana na mlinzi wa kampuni Jimson Security Company Ltd ya mkoani Iringa,na walikamatwa wakiwa wanasafirisha vifaa hivyo kwa kutumia pikipiki aina ya Boxer isiyo kuwa na namba ya usajili.

Mmoja wa wananchi katika kata ya Ingawa ,Lucy Andrea,amesema kuwa uwepo wa mradi huo umeleta ajira kwa wananchi wanaoishi maeneo ya jirani na mradi huo na mikoa ya jirani .

Aidha wananchi hao wameomba kukamilika kwa mradi huo mapema ili kuwaondolea adha ya upatikanaji wa maji kwa wananchi wilayani Mbarali.

Mradi huo wa Miji 28 ni mradi wa serikali wa kimkakati unaotekelezwa kwenye Mji wa Rujewa wilayani Mbarali chini ya kampuni ya Larsen & Toubro Limited, kwa zaidi ya billioni 50 na kutoa huduma kwa wananchi wa mikoa ya Mbeya na Njombe.

.