November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watu saba akiwemo mganga wa kienyeji watiwa mbaroni kwa tuhuma za mauaji

Judith Ferdinand,Timesmajira online, Mwanza

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linawashikilia watu 7 kwa tuhuma za kuhusika na matukio ya mauaji ya kupanga kutokana na imani potofu za kishirikina.

Akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbroad Mutafungwa, ameeleza kuwa wamefanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao kutokana na utendaji kazi wenye weledi wa hali ya juu wa Askari wa Idara ya Upelelezi, kitengo cha Uchunguzi wa Sayansi ya Jinai na Askari wa kazi za kawaida.

Pamoja na ushirikishwaji wa jamii katika kuwabaini na kuwatolea taarifa watu wanaojihusisha na matukio ya kihalifu katika maeneo wanayoishi, ambapo kabla na baada ya matukio hayo elimu ilitolewa kwa wananchi katika maeneo hayo.

Ambapo ameeleza kuwa miongoni mwa matukio ya mauaji ambayo watuhumiwa hao wanatuhumiwa kuhusika ni pamoja na lililotokea Mei 10,2023 majira ya saa 11:00 huko katika Kijiji cha Bugumangala, Kata ya Nyanguge Wilaya ya Magu.

Ambako ilipatikana taarifa ya tukio la maujia ya Ester Lukonu(51), mkulima na mkazi wa Kijiji cha Bugumangala aliyeuawa kwa kukabwa shingoni kisha kukatwa sehemu zake za siri na mwili wake kutelekezwa katika shamba la mihogo.

Kamanda huyo ameeleza kuwa katika tukio hilo ilionekana kuwa marehemu aliingiliwa kimwili kabla ya mauaji hayo ya kikatili kwani katika eneo la tukio ilipatikana kondomu iliyotumika,ambapo tukio hilo lilifanywa na watu ambao hawakuweza kufahamika mara moja.

Ameeleza kuwa watuhumiwa wote waliohusika katika tukio hilo walikamatwa na askari wa jeshi hilo waliobobea katika upelelezi wa makosa ya mauaji huku watuhumiwa hao wamehojiwa na kukiri kuhusika na mauaji hayo ya kikatili baada ya kumbaka Ester Lukonu kisha kumuua na kukata sehemu yake ya siri.

“Katika kundi la watuhumiwa hao amekamatwa pia mganga wa kienyeji aliyepokea sehemu ya siri ya marehemu kisha kuikausha kwa moto nakuisaga kwa ajili ya matumizi ya uganga kwa imani potofu za kishirikina,vielelezo mbalimbali katika kesi hiyo vimechukuliwa kwa ajili ya uchunguzi wa kitaalam,”.

Pia amewataja watuhumiwa waliokamatwa katika tukio hilo ni Masunga Mabula(32),mkulima na mkazi wa Nyanguge, Ezekiel Charles(45) mganga wa kienyeji na mkazi wa Kisamba wilayani Magu,Salome Raphael(32) mkulima,mkazi wa Kisamba, Kata ya Lububu.

Mutafungwa ameeleza kuwa katika tukio la pili lilitokea Aprili 26,2023 majira ya saa 6:30 usiku huko katika Kijiji cha Matale, Kata ya Bujashi, Wilaya ya Magu kuliripotiwa tukio la mauaji ya Katarina Luzali (48)mkulima na mkazi wa Kijiji cha Matale, aliyeuawa kwa kukatwa sehemu ya shingoni na kitu chenye ncha kali.

Huku watuhumiwa waliofanya tukio hilo hawakuweza kufahamika mara moja pia walimjeruhi mume wa marehemu huyo aitwaye Joseph Kanyasa(50),mkulima na mkazi wa Kijiji cha Matale kwa kumchoma na kitu chenye ncha kali sehemu za tumboni alipokuwa akijaribu kupambana nao.

Ambaye pia alifariki dunia akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sekou-Toure Mwanza ambapo chanzo cha tukio hilo ni imani potofu ambapo Katarina Luzali alikuwa akituhumiwa kijijini hapo kwa muda mrefu kujihusisha na vitendo vya imani za kishirikina.

Kamanda huyo ameeleza kuwa baada ya tukio hilo Askari wa jeshi hilo walifanya msako mkali na kuwakamata watuhumiwa wa nne kwa kuhusika na mauaji hayo.

Ambapo aliwataja watuhumiwa waliohusika na mauaji ya Katarina ni pamoja Eunice Lunzari(50),mkulima na mkazi wa Matale, Benard William (86),mkulima na mkazi wa Matale,Maguta Chandaruba(48),mkulima na mkazi wa Matale na Mashaka Maduka(43),mkulima na mkazi wa Matale.

Aidha Kamanda huyo ameeleza kuwa watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani mara baada ya uchunguzi utakapokamilika.

Jeshi hilo linatoa wito kwa wananchi wote kuacha kujihusisha na imani potofu za kishirikina ambazo zinachangia matukio ya kihalifu na mauaji badala yake wanawahimiza kufanya kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo kuliko kuendelea kudanganywa na waganga matapeli wenye lengo la kujipatia fedha kwakuendelea kuwaaminisha kuwa mafanikio yatatokana na ushirikina.