Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Mwanza
Watu 172 wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Nyamagana, mkoani Mwanza na kusomewa mashtaka kadhaa yakiwemo ya kuharibu mali, kuchoma moto na unyang’anyi wa kutumia silaha.
Watuhumiwa hao wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Oktoba 29 na 30 mwaka huu,wamefikishwa mahakamani Novemba 07, 2025 chini ya ulinzi wa Jeshi la Polisi na kusomewa mashitaka yanayowakabili kwa nyakati tofauti na kwa makundi kulingana na maeneo wanakodaiwa kutenda makosa hayo.
Akisoma mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Raula Shehagilo, Kiongozi wa Jopo la Waendesha Mashtaka wa Serikali, Jaines Kihwelo akisaidiana na Heleni Mabula na Sara Heperias amesema shtaka linalokabili kundi la kwanza linadaiwa kutenda kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha kinyume na kifungu cha 287(a) cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2023, kosa wanalodaiwa kulitenda Oktoba 30, mwaka huu.
Aidha, Mwendesha Mashtaka huyo wa Serikali amesema kwa nyakati tofauti watuhumiwa hao wakishirikiana na watu wengine ambao bado hawajakamatwa, wanashtakiwa kwa kosa la kuharibu mali kwa makusudi kinyume na kifungu cha 326 (1) cha Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 marekebisho mwaka 2023, kufanya fujo kinyume na kifungu cha 74(1) na cha (2) 76 na 37 cha Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 marejeo ya mwaka 2023.
Kosa lingine linalowakabili washtakiwa hao ni kuharibu mali, kosa wanalodaiwa kulitenda kinyume na kifungu cha 326(1) cha Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 marejeo ya mwaka 2023, kuchoma moto mali kinyume na kifungu cha 319 (a)(b) cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2023, kufanya maandamano bila kibali kinyume na kifungu cha74 (1)(2) 76 na 37 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2023.
Washtakiwa wote wamekana kutenda makosa hayo. Pia wamekosa dhamana kutokana na sehemu ya makosa yanayowakabili kutodhaminika na waheshimiwa mahakimu kwa nyakati tofauti wameelekeza washtakiwa hao kurudishwa rumande hadi kesi hiyo itakapoitwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa, Novemba 17, 19 na 20, mwaka huu.
Upande wa utetezi katika shauri hilo, unawakilishwa na Mawakili watano kutoka Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) Kanda ya Mwanza, wakiongozwa na Wakili, Erick Mutta akisaidiana na Lugano Kitangalala, Emmanuel John, Salehe Nassoro na Debora Marwa,ambapo kwa nyakati tofauti waliomba mahakama kuhimiza upande wa Jamhuri kukamilisha upelelezi wa makosa yanaowakabili wateja wao kwa wakati.
Miongoni mwa mashtaka waliyosomewa na yasiyodhaminika ni pamoja na kosa la unyang’anyi huku washitakiwa wakirejeshwa rumande hadi Novemba 17, 19, 20 na 21, 2025 watakapofikishwa tena kortini kusomewa maelezo ya awali (PH).

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi