Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
JESHI la Polisi Kikosi cha Polisi Reli limewakamata watu 13 wanaodaiwa kuharibu miundombinu ya reli ya kisasa (SGR) na kuiba nyaya za Shirika la Reli Tanzania (TRC) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Kamanda wa Kikosi cha Polisi Reli nchini, Gallus Hyera alisema hayo Jana wakati akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam.
Alisema watuhumiwa hao tayari wamefikishwa katika Mahakama na wanakabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi.
Kamanda Hyera alisema kati yao watuhumiwa nane wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha na watuhumiwa watano wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni.
Alibainisha kuwa mmoja kati ya watuhumiwa hao ni fundi umeme na muajiriwa wa kampuni ya YAPI MERKEZI inayotekeleza jenzi wa miundombinu ya SGR ambaye huwa anakata nyaya maeneo mbalimbali.
Alisema Novemba 28, 2024 majira ya mchana huko maeneo ya Mdaula mkoani Pwani watuhumiwa watano walikamatwa wakiwa na kilo saba za nyaya za shaba.
Alieleza kuwa Novemba 30, 2024 maeneo ya Visiga wilaya ya Mlandizi kwenye Kampuni ya The African Light Investment Ltd inayomilikiwa na raia wa kigeni (China na Kenya) zilikamatwa Nyaya za shaba zenye uzito wa Kilo 882.5.
Pia Jeshi lilimkamata Paulo Joseph ambaye ni wakala wa kutafuta na kuharibu Miundombinu ya miradi ya serikali. Desemba 2, 2025 mkoani Pwani ulifanyika upekuzi kwenye nyumba inayomilikiwa na wamiliki wa The African Light Investment Ltd (Raia wa China na Kenya).
“Katika upekuzi huo, watuhumiwa walikutwa na nyaya mbalimbali za shaba zenye uzito wa Kilogramu 3687.9. Nyaya hizo zimetambuliwa kuwa zimetokana na uhalibifu kwenye miradi ya SGR na
TANESCO jumla wamekutwa na Nyaya Kilo 4,570.4 pamoja na raw copper bars 44 zenye uzito wa Kilo 971.5,” alisema Hyera.
Alisema Desemba 4, 2024 huko Kisemvule Pwani kufuatia taarifa za kiintelijensia zilikamatwa Nyaya za shaba Kilo 608.6 Mali ya TANESCO na Kilo 37 Mali ya SGR na Flat Bars zilizozalishwa kwa kuyeyushwa nyaya za shaba Kilo 5,517.4 kwenye kiwanda cha chuma chakavu cha Metal Chem International.
Hyera alisema Desemba 5, 2024 huko maeneo ya Mwenge Dar-es-salaam zilikamatwa Copper Wire Kilo 65.5 toka kwa wanunuzi wa chuma chakavu pamoja na waya wa shaba wenye uzito wa kilo 6.5 wakiwa katika harakati ya kuuza.
Aidha alitoka onyo kwa mtu yeyote anayejipanga kufanya uhalifu huo wa kukata
nyaya za shaba kwenye miradi ya SGR na TANESCO na kusisitiza kuwa operesheni bado inaendelea.
Hyera aliwataka wanunuzi wa vyuma chakavu kuacha kununua Nyaya za shaba zinazotokana na uhalibifu wa miundombinu ya Serikali.
More Stories
Waziri Mavunde:Benki Kuu yanunua tani 2.6 za Dhahabu nchini
Kampeni msaada wa kisheria ya mama Samia kutatua kero za kisheria Katavi
Wizara ya madini yakusanya bil.521 nusu ya kwanza mwaka wa fedha 2024/25