November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watoto wenye mtindio wa ubongo tusiwanyanyapae

KATIBA ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 11 vifungu vidogo vya (1) – (3) inazungumzia haki ya kupata elimu kwa raia wa Tanzania bila ya kubaguliwa huku mamlaka ya nchi ikitakiwa kuweka utaratibu utakaowezesha kupatikana kwa haki hiyo.

Haki hiyo inatokana na umuhimu wa elimu kuwa ni wa kipekee kwa kila binadamu ambapo inasisitizwa haki hiyo kutolewa bila ubaguzi wala unyanyapaa wa aina yoyote na kila raia ana haki ya kupewa fursa ya kutafuta elimu katika fani aipendayo hadi kufikia upeo wowote kulingana na stahili na uwezo wake.

Ni wazi katiba ya nchi ndiyo sheria mama katika nchi yoyote hapa duniani, hivyo mtu ye yote anayekwenda kinyume na matakwa ya katiba anakuwa ametenda kosa na hivyo kustahili kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria za nchi zilizopo.

Hata hivyo hapa nchini bado tuna changamoto kubwa ya watu wengi kutoielewa katiba ya nchi yao na hivyo kushindwa kuchukua hatua zozote za kisheria inapotokea wamenyimwa haki zao za msingi kwa mujibu wa katiba.

Moja ya watu wanaoathiriwa na uelewa mdogo wa jamii katika kuielewa katiba ya nchi, ni kundi la watoto wenye ulemavu wa mtindio wa ubongo ambao wengi wao wamekuwa wakinyimwa haki ya kupata elimu kutokana na hali ya ulemavu walionao.

Baadhi ya wazazi ama walezi wa watoto wenye mtindio wa ubongo hapa nchini hudiriki kuwaficha watoto hao ndani na mara nyingi huwaweka kwenye mazingira machafu kiasi cha kuhatarisha afya zao ili kukwepa tu jamii isielewe kwamba wana watoto wenye matatizo ya akili.

Tukitupia macho Sera ya elimu ya mwaka 2014 hapa nchini na ile ya watu wenye ulemavu zote zinasisitiza umuhimu wa watoto wenye ulemavu wa aina yoyote kutobaguliwa katika suala zima la kupata elimu hii ni pamoja na kutonyanyapaliwa.

Sera hiyo inasisitiza upatikanaji wa elimu ya awali na ya msingi kwa watoto wote wenye umri wa miaka saba na kwamba watoto wenye ulemavu watapewa kipaumbele. Pamoja na azma hii mfumo wa elimu hautoi fursa kwa watoto wenye ulemavu kupata elimu bila vipingamizi.

Tamko la Sera linaeleza kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine itaweka mazingira yatakayohakikisha kwamba watoto wenye ulemavu wanapata elimu jumuishi kwa kuzingatia mahitaji yao maalum lakini ukichunguza hakuna utekelezaji wa maana unaofanyika kuhusu tamko hili.

Tutupie macho pia sehemu ya Mkataba wa Haki za Watu wenye Ulemavu ambao nchi yetu ya Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizousaini na kuuridhia ambao katika ibara yake ya 24 unazungumzia haki ya elimu kwa watoto wenye ulemavu.

Ibara hiyo inaeleza, nanukuu; “(1) Watu wote wana haki ya kupata elimu, nchi zitahakikisha kwamba mfumo mzima wa elimu unajumuisha watu wenye ulemavu, na kwamba mfumo wa uelimishaji unaeleza,”

“(2) Ili kuyafanikisha haya, nchi zitahakikisha kuwa watu wenye ulemavu, (a) Hawatengwi kielimu kutokana na ulemavu wala kunyimwa fursa ya elimu bure ngazi ya msingi na sekondari kutokana na hali waliyonayo, (b) Wanachagua aina ya elimu inayojumuisha na kupatikana kwenye jamii waishimo,”

“(c) Wanafanyiwa marekebisho ya kuridhisha kwenye mazingira jenzi ili kuhakikisha kuwa wananufaika na elimu kwa kadri inavyowezekana na (d) wanapata msaada wanaouhitaji ili kunufaika kielimu.”

Hata hivyo pamoja na uwepo wa sera na sheria ya watu wenye ulemavu hapa nchini bado shule takriban zote za awali/msingi/sekondari na vyuo vya elimu ya juu vimejengwa bila kuzingatia mahitaji maalumu ya watoto wenye ulemavu.

Vilevile hata upande wa mafunzo ya walimu na mitaala ya shule haizingatii mahitaji maalumu ya watu wenye ulemavu, kwa mfano matumizi ya lugha ya alama na maandishi ya nukta nundu hali inayochangia kwa kiasi kikubwa idadi ya watoto wenye ulemavu wanaoandikishwa darasa la kwanza kuwa chini ya asilimia moja.

Tanzania ni moja ya nchi ambazo zimekuwa zikijihusisha na mipango mbalimbali ya Kitaifa na Kimataifa inayohusu masuala ya ulemavu ambapo Kimataifa imesaini mikataba kuhusu watu wenye ulemavu ikiwemo mikataba ya Haki kwa watu wenye Ulemavu (1975) na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za mtoto (CRC) wa mwaka 1989.

Pia mkataba wa Haki na Fursa sawa kwa Watu wenye Ulemavu wa mwaka 1993 na kwa upande wa barani Afrika, Tanzania ni miongoni mwa nchi waasisi wa Mpango wa utekelezaji wa muongo wa Watu wenye Ulemavu na mwanachama wa Taasisi ya Marekebisho kwa Watu wenye Ulemavu (African Rehabilitation Institute – ARI).

Wakati serikali ikishindwa kutimiza wajibu wake kwa watoto wenye ulemavu hasa upande wa watoto wenye mtindio wa ubongo hata jamii yenyewe bado ni changamoto kubwa kwa watoto hawa kutokana na kutengwa ama kunyanyapaliwa ndani ya familia na mara nyingi wengi wao hufichwa kwa kufungiwa ndani ili wasionekane.

Inaonesha wazi bado panahitajika nguvu ya ziada katika kupaza sauti ya pamoja ili kuwasaidia watoto hawa wenye mtindio wa ubongo ambao bado wako kwenye vifungo visivyo rasmi kwenye makazi ya wazazi ama walezi wao.

Bado baadhi ya jamii kutokana na mila na desturi wanaamini mtoto anayezaliwa akiwa na mtindio wa ubongo ni laana na huwapa majina yasiyofaa, mfano, taahira, mwehu ama zezeta, hali inayopaswa kukemewa kwa nguvu zote na tuwaone sawa watoto hawa kama walivyo watoto wengine wasio na mtindio wa ubongo.

Mtoto Maganga Bundala (14) (siyo jina halisi) mkazi wa kata ya Kitangiri manispaa ya Shinyanga ni mmoja wa watoto wenye mtindio wa ubongo ambaye ni muhanga wa vitendo vya ukatili wa kufungiwa ndani na wazazi wake kwa kipindi kirefu kabla ya kukombolewa na msamaria mwema.

Maganga ambaye kwa sasa ni miongoni mwa wanafunzi 10 wenye mtindio wa ubongo wanaolelewa na kituo cha Triest Children with Disability kilichopo kata ya Kitangiri manispaa ya Shinyanga alikombolewa kwenye kifungo cha ndani mwaka 2017.

Mkurugenzi wa kituo cha Triest, Valentine Maziku anasema, “…Kupatikana kwa mtoto huyu ni baada ya sisi kwenda nyumbani kwao tukiwa katika utaratibu wa kawaida wa kuwatembelea waumini wetu kwa lengo la kuwajulia hali,”

“Hata hivyo tukiwa ndani tunaendelea na maongezi na wenyeji wetu tulisikia ndani ya chumba kimoja kuna kama mtu anagonga gonga mlango kwa nguvu, niliuliza kulikoni, kuna mtoto mwingine akanijibu haraka haraka kwamba ni Maganga amefungiwa ndani, nilishituka sana.”

Maziku anaendelea kueleza kuwa baada ya kuelezwa kuna mtu amefungiwa ndani walimuomba mama mwenye nyumba amfungulie mtu aliyemfungia ndani lakini aligoma kwa madai ni mgonjwa na hana akili nzuri.

Anasema waliendelea kushinikiza mpaka wakafanikiwa na kwenda katika chumba alichokuwa amefungiwa Maganga na kumkuta akiwa katika mazingira machafu kutokana na chumba kutofanyiwa usafi mara kwa mara.

“Kwa kweli tulisikitishwa na hali tuliyomkuta nayo mtoto huyu, ilibidi niwaombe wazazi wake tumtoe nje, tulishangaa baada ya kutoka nje alipiga yowe kubwa sana ikabidi tumrudishe ndani ambako niliomba maji na kumuogesha mwili wote, na nilitafuta nguo nikamvalisha,”

“Niliwauliza wazazi wake kwa nini walikuwa wakimfungia ndani, majibu yao hayakunipendeza, walidai ni mwehu, wakimuacha nje anaweza kwenda hovyo, niliwaomba nimchukue waligoma na kunishauri kama ni msaada wa malezi basi nimchukue nduguye mwenye akili timamu, nikasema hapana, mimi namtaka Maganga,” anaeleza Maziku.

Anaendelea kueleza kuwa baadae wazazi walikubali lakini hata hivyo ilibidi amuache mtoto huyo palepale kwao ambapo alimpelekea godoro la kulalia na kwa kipindi cha miezi miwili alikuwa akienda kila siku asubuhi kumfanyisha mazoezi huku akimpaka mafuta ya Vaseline mwilini kwa lengo la kulainisha ngozi yake iliyokuwa imekakamaa.

“Baada ya miezi miwili nilianza kwenda naye ofisini kwangu ambako kidogo kidogo nilianza kumfanyisha mazoezi ya kuongea na kumwelekeza jinsi ya kujisaidia pale anaposhikwa haja ndogo ama kubwa, mwishowe aliweza kujihudumia yeye mwenyewe,”

“Ilibidi niwe nikimfuata kwao kila siku asubuhi na kumrudisha jioni, muda mfupi wazazi wake walipigwa na mshangao walipoona anaweza kuzungumza japo kwa shida, na sasa kwa siku za Jumamosi na Jumapili wanaweza kumuachia nyumba akailinda bila hofu yoyote pale wanapokuwa wameenda kwenye shughuli zao za kutafuta riziki,” anaeleza Maziku.

Anasema baadaye yeye na wenzake waliamua kuanzisha kituo kwa ajili ya kuwasaidia watoto wenye mtindio wa ubongo wanaoishi katika kata ya Kitangiri ambapo walifanikiwa kupata watoto 17 ambao walianza kuwapatia mafunzo mbalimbali ikiwemo kuwajengea uwezo wa kuzungumza kwa ufasaha.

“Huwezi amini ndani ya kipindi cha mwaka mmoja watoto hawa wamekuwa na mabadiliko makubwa, tumewafundisha mambo mengi ikiwemo kuhesabu, kuandika na kusoma na baadhi wanaweza kufanya kazi za mkono, mfano Maganga anabrashi vizuri viatu, na baadhi wanapika maandazi wao wenyewe,”

“Hali zao kwa sasa zinaridhisha ikilinganishwa na hapo awali tulipowachukua makwao, wengi hawakuwa hata na uwezo wa kujieleza, sasa wanazungumza vizuri, na wamekuwa wasumbufu katika kuuliza maswali mengi wakitaka kufahamu mambo mengi kwa wakati mmoja, ni hatua nzuri,” anaeleza Maziku.

Mkurugenzi huyo anaendelea kueleza kuwa watoto hao siyo kwamba hawana akili kama wanavyotazamwa na baadhi ya watu, bali uelewa wao ni mdogo tu ambapo wanapopatiwa mafunzo ya kina wana uwezo wa kuelewa mambo mengi kama wanavyoelewa watoto wengine wasio na mtindio wa ubongo.

“Mfano mzuri, ni huyu mtoto Maganga, siku moja nilikuwa nimekaa naye akaniuliza swali moja kwa utaratibu, Mwalimu mbona sisi hapa hatufanyi mahafali kama wanavyofanya wenzetu kwenye shule nyingine? Ukweli nilishangaa nikawaza kapata wapi wazo hilo,”

“Nikaamini alikaa na kufikiri iweje wao hawatendewi kama wanavyotendewa wenzao, aliamini hata wao wanastahili kufanyiwa mahafali kama wanavyofanyiwa wenzao, niliwashirikisha viongozi wenzangu na tukafanyia kazi wazo lake, na kwa mwaka huu tumeweza kufanya mahafali ya kwanza katika kituo chetu, ambapo watoto wameweza kuonesha kazi zao za mikono walizofanya wenyewe,” anaeleza.

Anaendelea kueleza kuwa kwa upande wa watoto wa kike waliopo kwenye kituo hicho hivi sasa wanaweza kupika baadhi ya vyakula na hata kuosha vyombo bila tatizo tofauti na hapo awali walipopelekwa kituoni hapo wakiwa hawaelewi chochote.

Maziku anasema kuna kila sababu ya jamii kuendelea kuelimishwa juu ya kutowatenga ama kuwaficha watoto wenye ulemavu wa mtindio wa ubongo na badala yake wawapeleke shule ama kwenye vituo vinavyotoa malezi kwa watoto hao ili waweze kupatiwa elimu na mafunzo mengine yatakayowasaidia baadae.

Pia anaishauri serikali iangalie uwezekano wa kuendesha kampeni maalumu ya kuwaibua watoto wote wenye mtindio wa ubongo waliopo hapa nchini ili waweze kupatiwa elimu kama inavyofanyika kwa makundi mengine ya watoto wenye mahitaji maalumu.

“Nafikiri ifike wakati serikali iweke utaratibu utakaowezesha kutambulika kwa watoto wenye mtindio wa ubongo popote pale walipo na pawe na mipango ya makusudi ya kuwatengea shule maalumu badala ya kuwachanganya na watoto wengine maana wao wanahitaji uangalizi wa karibu pale wanapofundishwa,” anaeleza Maziku.

Akizungumzia kuhusu changamoto anazokutana nazo katika kuwahudumia watoto hao, Maziku anasema moja ya changamoto ni baadhi ya wazazi ama walezi kuamua kuwachukua watoto wao kwa kisingizio wanawapeleka katika shule za bweni wakati sivyo.

Lakini pia uhaba wa fedha kwa ajili ya kuwahudumia watoto hawa na ukosefu wa eneo la kutosha la kuweza kujenga kituo kikubwa chenye uwezo wa kuchukua watoto wengi ambapo kwa sasa kituo kinaendeshwa kwa msaada wa Parokia ya kanisa katoliki Kitangiri Shinyanga na kusaidiwa na Paroko Raphael Islahim.

“Tunaamini bado serikali ina wajibu wa kuendesha sensa maalumu hapa nchini ili kuwatambua watoto wote wenye ulemavu wa mtindio wa ubongo, wapo wengi isipokuwa hapajafanyika juhudi za kuwatafuta, wengi wao wamefichwa majumbani katika vifungo visivyo rasmi ili wasionekane na watu, lakini wanaofanya hivyo waelewe huo nao ni ukatili,”

“Kwa hapa kwetu nitoe wito kwa wadau watakaowiwa kuona jinsi gani wanaweza kutusaidia ikiwemo kuwapatia nguo na chakula watoto hawa wasisite kujitokeza, lakini pia jamii iache kutuona sisi kama kituko, baadhi hutucheka eti tunaishi na wehu, kauli hizi hazifai, tushikamane pamoja kuwasaidia watoto hawa, ni binadamu kama sisi,” anaeleza Maziku.