Judith Ferdinand, Mwanza
KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Mwanza ACP Muliro Jumanne amesema kuwa, jana saa 11 alfajiri jeshi hilo limewaokota watoto wawili waliokuwa wametupwa kwenye shamba la mpunga/majarubani katika mtaa wa Mtakuja Kata ya Nyamhongolo Wilaya ya Ilemela Mkoani hapo.
Katika tukio hilo mtoto wa kwanza mwenye jinsia ya kiume anakadiriwa kuwa na mwaka mmoja akiwa amevalishwa fulana ya rangi ya blue huku wa pili mwenye jinsia ya kike anayekadiriwa kuwa na umri wa miezi mitatu akiwa amevalishwa nguo moja mwili wote rangi nyeupe.
Kamanda Muliro amesema, watoto hao wamekutwa wakiwa katika mazingira magumu lakini wakiwa hai, huku akikemea kitendo cha kuwatupa watoto hao kwani ni miongoni mwa makosa makubwa ya kikatili dhidi ya watoto na hakivumiliki.
Hata hivyo amesema, watu wote waliohusika na tukio hilo watasakwa popote walipo, watakamatwa na kufikishwa mahakamani na watoto wamepelekwa hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa matibabu na hali zao zinaendelea vizuri.
Aidha jeshi hilo linatoa wito kwa wananchi kuwa na uvumilivu wanapokuja na migogoro ya kifamilia na wapende kuhusisha vyombo vya kisheria kama Taasisi za kidini katika kusaidia kutatua migogoro hiyo.
More Stories
DC Korogwe awataka viongozi wa vijiji kuwatumikia wananchi kwa uadilifu
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam