Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online, Dar
WATOTO wanaoishi na kufanyakazi mitaani wamepongeza hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Railway Children Africa kwa kushirikiana na Taasisi ya Baba Watoto kwa lengo la kuwawezesha kufikia ndoto zao.
Taasisi hizo kwa pamoja zinatekeleza Mradi wa USAID-Kizazi Kipya.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki, watoto hao wamesema changamoto nyingi ambazo walikuwa
wanakumbana nazo siku za nyuma zimepata ufumbuzi.
Wamesema tayari baadhi yao wameanza kupatiwa mafunzo katika vyuo vya VETA na wengine wakiwa kwenye mchakato huo.
Mmoja wa watoto hao, Abel John, amesema miongoni mwa changamoto
walizokuwa wakikumbana nazo ni pamoja na kubamkiziwa kesi pindi
walipokamatwa na Polisi.
Amesema Railway Children Africa imekuwa ikiwapatia msaada wa kisheria. Ametaja changamoto nyingine kuwa ya kuugua, ambapo awali ilikuwa ngumu kupata matibabu.
Kwa mujibu wa John kwa sasa wakiugua wanapatiwa ma matibabu kupitia mradi huo wa Baba Watoto.
Mtoto Mwingine,Peter Paul amesema kuna wakati alikuwa anaumwa
sana na kwamba kama isingekuwa taasisi hiyo leo asingekuwa hai.
Pia amesema wanapatiwa chakula, maji ya kuoga na mahitaji mengine
muhimu hatua, huku wakiandaliwa kuweza kufukia ndoto zao.
Kwa upande wake Afisa Mawasiliano wa Railway Children Africa, Henry Mazunda, amesema wamekuwa wakifanyakazi zao kupitia ngazi tatu.
Amesema ngazi ya kwanza ni ya kuwafuata watoto wanaoishi na
kufanyakazi mitaani na kuwapatia mahitaji muhimu na ya haraka.
Ametaja baadhi ya mahitaji hayo kuwa ni pamoja na msaada wa kisheria, chakula na kufanya jitihada za kuwaunganisha na familia zao pamoja na kuendelea kuwapatia mahitaji yao muhimu ikiwemo chakula pamoja na mahitaji ya shule.
Ngazi nyingine ni kuelimisha jamii ili iweze kutambua kuwa watoto
wanaoishi na kufanyakazi mitaani wana haki sawa na watoto wengine,
hivyo hawana sababu ya kuwaona kama watu wabaya.
“Watoto hawa wanaondoka nyumbani kwa sababu mbalimbali ikiwemo wazazi kutengana, kukosa mahitaji maalum kwa sababu za umaskini, pamoja na ukatili,kwa hiyo watoto hawa wanahitaji kusaidiwa,”amesema.
Amesema taasisi hiyo inafanyakazi katika mikoa saba baada ya kufanya utafiti na kubainika ndiyo yenye watoto wengine. Hadi sasa taasisi hiyo imeishahudumia watoto zaidi ya 10,000.
More Stories
Wananchi Kisondela waishukuru serikali ujenzi shule ya ufundi ya Amali
RC.Makongoro ataka miradi itekelezwe kwa viwango
LALJI yatoa msaada wa sare na vifaa vya shule kwa yatima