Na Allan Kitwe,Timesmajiraonline,Nzega
WATOTO wa kike wanaosoma katika shule za sekondari Wilayani Nzega Mkoani Tabora wamehamasishwa kusoma masomo ya sayansi ili kuongeza idadi ya wataalamu wa fani mbalimbali hapa nchini.
Rai hiyo imetolewa jana na Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Winfrida Funto kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo Naitapwak Tukai alipokuwa akifungua semina ya umuhimu wa masomo ya sayansi kwa mtoto wa kike kwa wadau wa elimu.
Funto ameeleza kuwa masomo ya sayansi ni muhimu yafundishwe kwa watoto wa kike na wa kiume kwa kuwa wana fursa sawa za ajira na taifa lina uhitaji mkubwa wa wataalamu wa sayansi.
Amepongeza Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF) kwa kuendesha semina hiyo kwa Wakuu wa shule za sekondari, Maafisa Elimu Kata, Wenyeviti wa Bodi za shule na wazazi ili wakahamasishe wasichana kupenda masomo hayo.
“Nawapongeza sana UNICEF kwa kushirikiana na serikali ya Canada na Tanzania kwa kufanikisha semina hii,naomba sana wote mliopata fursa ya kushiriki semina hii mkawasaidie watoto wa kike kupenda masomo ya sayansi,”amesema.
Funto amesisitiza kuwa watoto wa kike wana uwezo mkubwa wa kusoma masomo hayo, wasibaguliwe wala kukatishwa tamaa bali wajengewe mazingira mazuri ya kupenda masomo hayo ili kuongeza idadi ya wataalamu wa kike.
Mratibu wa Mradi wa UNICEF Wilayani hapa Flora Shiwa amesema kuwa semina hiyo ni muhimu sana kwa kuwa watoto wa kike katika Mkoa bado wako nyuma sana kusoma masomo hayo na wengine wanayaogopa.
Amepongeza juhudi kubwa zinazoendelea kufanywa na shirika hilo ikiwemo kuendesha semina kwa wadau wa elimu, kutoa vifaa vya TEHAMA na maabara katika shule za sekondari ili kuhamasisha wasichana kupenda masomo ya sayansi.
“Walimu wakuu wa shule, Maafisa Elimu Kata, Bodi za Shule, wazazi na walezi wa watoto kuweni mstari wa mbele kuhamasisha watoto wa kike kusoma masomo haya ili kuongeza idadi ya wataalamu wa kike katika sekta zote,”ameeleza.
Akitoa semina kwa wadau hao Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma Dkt.Huruma Bwagilo ameeleza kuwa huu ni wakati wa mabadiliko ya teknolojia hapa duniani, hivyo ni muhimu sana kwa mtoto wa kike kuwa sehemu ya mabadiliko haya.
Amebainisha kuwa wataalamu wa kike waliosoma sayansi wanahitajika sana katika sekta mbalimbali ikiwemo ualimu, udaktari, uhandisi, uuguzi, urubani na kadhalika.
Mwalimu Vaileth Bonosi ambaye ni Afisa Elimu wa Kata ya Nata katika Wilaya ya Nzega amesema kuwa masomo ya sayansi sio magumu kama baadhi ya watoto wa kike wanavyodhania, hayo ni maneno ya kuwakatisha tamaa tu.
Ameomba walimu, wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuendelea kuwatia moyo watoto wa kike ili kuwaongezea ari ya kupenda masomo hayo ya STEM yaani Sayansi, Teknolojia, Engineering (Uhandisi) na Mathematics (Hisabati).Â
More Stories
Kampeni msaada wa kisheria ya mama Samia kutatua kero za kisheria Katavi
Wizara ya madini yakusanya bil.521 nusu ya kwanza mwaka wa fedha 2024/25
Meya awafunda wenyeviti Serikali za Mitaa