Na.Mwandishi wetu,timesmajira,Dodoma
Jumla ya watoto 12,131,049 sawa na asilimia 117.8 wamepatiwa chanjo ya matone dhidi ya ugonjwa wa Polio kwa watoto chini ya miaka mitano kati ya watoto 10,295,316 waliolengwa kwenye kampeni ya Chanjo iliyofanyika nchini tarehe 18 hadi 21 Mei mwaka huu.
Hayo yamebainishwa leo na Waziri wa Afya Mhe.Ummy Mwalimu wakati akitoa tathimini ya kampeni ya chanjo ya matone dhidi ya Ugonjwa wa Polio kwa watoto chini ya miaka mitano nchini kwenye viwanja vya Bunge jijini Dodoma.
Waziri Ummy amesema idadi hiyo iliyofikiwa ni mafanikio makubwa kama nchi na kutoa pongezi kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya,Timu za uendeshaji wa huduma za afya ngazi ya Mikoa na Halmashauri ,watumishi wa afya pamoja na wadau mbalimbali wakiwemo wadau wa maendeleo kwa kusimamia kikamilifu maandalizi ,uzinduzi na utekelezaji wa kampeni katika maeneo yao kwa umahiri mkubwa.
“Nawapongeza pia wazazi na walezi wote kwa kuitikia wito wa Serikali kwani afua ya chanjo ni muhimu kwa watoto katika kuwalinda dhidi ya magonjwa yanayo zuilika kwa chanjo”.
Waziri Ummy aliutaja Mkoa wa Ruvuma umeongoza kwa kuvuka lengo kwa 131%, ikifuatia na Shinyanga 128%, Rukwa 123%, Pwani 122%, Arusha 122%, Mbeya, Geita, Dar es Salaam na Simiyu yote ina 121%, Singida, Dodoma na Tabora 118% , Kigoma, Njombe, Katavi 117%, Morogoro 116%, Mara, Mtwara, Lindi na Tanga 115%, Kilimanjaro na Mwanza 114%, Manyara na Iringa 113%, Songwe na Kagera 111%.
Hata hivyo Waziri Ummy ametoa wito kwa Viongozi,wadau na wazazi kutoa ushirikiano kwa kampeni zinazofuata ambazo zinatarajiwa kufanyika mwezi Julai na Agosti mwaka huu.
Ameongeza kuwa tunayo kila sababu ya kuilinda nchi yetu na watoto wetu dhidi ya ugonjwa wa Polio.’Mzazi/Mlezi hakikisha watoto wanapata chanjo ya Polio,bado tunaweza kutunza rekodi ya Tanzania kuwa nchi isiyokuwa na ugonjwa wa Polio duniani.
Kampeni ya Polio inatakiwa kufanyika kila baada ya wiki nne ili kuhakikisha watoto wote wanafikiwa kulingana na mwongozo wa WHO wa kukabiliana na ugonjwa wa Polio unaelekeza kuwa endapo mlipuko wa ugonjwa umetoke nchi ambayo mlipuko umetokea pamoja na zile zinazozunguka zinapaswa kufanya kampeni za kutoa chanjo ya polio mara nne mfululizo pamoja na kutoa chanjo kwa watoto wote walio chini ya miaka mitano ili kuzuia kusambaa kwa maambukizi ya ugonjwa huu.
More Stories
NAOT watakiwa kuendana na viwango vya ukaguzi
Rais Samia kuzindua mfuko wa kuendeleza kazi za wabunifu
Makalla ampongeza Lissu kukiri CHADEMA haina wagombea Serikali za Mitaa