January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Picha ya Mtanda0

Watoto milioni 116 kuzaliwa kipindi hiki cha Corona duniani

NEW YORK, Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) linakadiria kuwa, watoto milioni 116 watakuwa wamezaliwa wiki 40 tangu ugonjwa wa virusi vya Corona (COVID-19) utangazwe kuwa janga la kimataifa Machi 11,mwaka huu.

Hayo yalibainishwa jana kupitia taarifa ya UNICEF iliyotolewa jijini New York, Marekani.

“Wanawake waliojifungua na watoto wachanga watakumbana na machungu mapya ikiwemo hatua za kuzuia kuchangamana, vituo vya afya kuzidiwa uwezo wa kutoa huduma, ukosefu wa vifaa vya matibabu, uhaba wa wahudumu wa afya wenye stadi za kutosha kwa kuwa wengi wanahudumia wagonjwa wa Corona sambamba na amri za kutotembea hovyo,”ilifafanua sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Henrietta Fore alinukuliwa katika taarifa hiyo akieleza kuwa, mamilioni ya wazazi duniani kote wanaanza safari ya uzazi kama ilivyokuwa akisema kuwa,wanalazimika kujiandaa kuleta kiumbe duniani katika dunia ambayo kwao, wajawazito wanahofia kwenda vituo vya afya.

“Ni kwa hofu ya maambukizi au wanakosa huduma ya dharura kutokana na vituo vya afya kuzidiwa uwezo au kutokana na amri ya kutotembea hovyo,îalibainisha.

Mkurugenzi Mtendaji huyo alieleza kuwa, ni vigumu kufikiria ni kwa jinsi gani ugonjwa wa Corona umeathiri uzazi na hivyo UNICEF inaonya kuwa,hatua za kuzuia watu kutoka majumbani mwao zinaweza kuvuruga huduma za afya za kuokoa maisha kama vile huduma za kujifungua na hivyo kuwaweka mamilioni ya wajawazito na watoto wao hatarini.

UNICEF inaeleza kuwa, nchi zinazotarajiwa kuwa na idadi kubwa ya watoto miezi tisa baada ya COVID-19 kutambuliwa kuwa ni janga ni pamoja na India watoto milioni 20.1, China watoto milioni 13.5, Nigeria watoto milioni 6.4 huku Pakistan ikitarajia watoto milioni tano na Indonesia watoto milioni nne.

Shirika hilo lilieleza kuwa, idadi kubwa ya mataifa hayo tayari yana viwango vya juu vya vifo vya watoto wachanga, hata kabla ya janga la COVID-19 na hivyo viwango hivyo vinaweza kuongezeka wakati huu wa Corona.

Marekani nayo ambayo imeathiriwa na janga la Corona inatarajia zaidi ya watoto milioni 3.3 kuzaliwa kati ya Machi 11 hadi Desemba, mwaka huu ambapo mamlaka za jimbo la New York, zinaangalia mbinu ya kuweka vituo vya kujifungulia kwa kuwa wajawazito wengi wanahofia kwenda kujifungulia hospitalini.

UNICEF inaonya kuwa ingawa ushahidi unaonesha kuwa wajawazito hawaathiriwi zaidi na COVID-19 kama ilivyo kwa watu wengine, serikali zinapaswa kuhakikisha kuwa bado wanapata huduma za kabla ya kujifungua, za kujifungua na baada ya kujifungua.

ìVivyo hivyo watoto wachanga wanahitaji huduma za dharura. Familia mpya zinahitaji msaada kuanza kunyonyesha watoto na kupata dawa, chanjo na lishe ili watoto wao wawe na afya,îiliongeza taarifa hiyo.

Aidha, UNICEF inatoa wito kwa serikali na wahudumu wa afya kuokoa maisha katika miezi ijayo kwa kuchukua hatua ikiwemo, kusaidia wajawazito kupata huduma za uchunguzi kabla, wakati na baada ya kujifungua na huduma zitolewe na wahudumu wenye ujuzi.

Pia kuhakikisha wahudumu wa afya wana vifaa vya kujikinga na wanapatiwa kipaumbele katika kupima iwapo wana virusi vya Corona au la na pia iwapo chanjo dhidi ya Corona ikipatikana, wawe wa kwanza kupatiwa ili waweze kutoa huduma bora.

Shirika la UNICEF linataka pia kuwepo kwa hakikisho la mbinu za kukinga na kudhibiti maambukizi ya virusi vya Corona kwenye vituo vya afya wakati wa kujifungua na baada ya hapo.

Pia kuwezesha wahudumu wa afya kutembelea wajawazito na wazazi majumbani mwao bila kusahau kutumia teknolojia kama vile simu kufikia wazazi walio maeneo ya ndani zaidi.