December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watoto 100 kupimwa moyo bure

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya

ZAIDI ya watoto 100  katika Mikoa ya Nyanda za juu Kusini wanatarajiwa kupatiwa vipimo vya upimaji  moyo bure pamoja na matibabu kutoka  Taasisi ya I Heart Tanzania kwa kushirikiana na hospitali ya Rufaa kanda ya Mbeya.

Imeleezwa kuwa huduma hiyo ya vipimo itakuwa  inapatikana hospitali ya Rufaa kanda ya Mbeya ambako kumewekwa  Kambi ya siku tatu  ambayo imeanza March 10 mwaka huu ambapo Taasisi ya I Heart Tanzania  inayojishughulisha na upimaji wa moyo kwa watoto itatoa huduma hiyo ya  uchunguzi na upimaji  wa moyo  kwa watoto chini ya umri wa miaka 14 kwa kushirikiana na hospitali ya rufaa kanda ya Mbeya

Akizungumza wakati  wa zoezi hilo Dkt. Nuru Mniwa Mkuu wa Idara ya Watoto Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya amesema lengo la kambi hiyo ya siku tatu ni kutoa huduma ya uchunguzi na vipimo kwa watoto chini ya umri wa miaka 14 ili kutambua matatizo mbalimbali ya moyo yanayowakumba pamoja na kuwapuguzia gharama za kusafiri umbali mrefu kutafuta kwenda kupata huduma hiyo. 

“Hii changamoto ni kubwa  na uwezekano wa watoto hawa kufika Taasisi ya Moyo ya JKCI pale wanapobainika na tatizo moyo kutokana na umbali na gharama za kujikimu” amesema Dkt. Mniwa

Naye  Dkt. Gloria Mbwile, Daktari Bingwa Mbobezi wa magonjwa ya Moyo kwa watoto Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya amefafanua kuwa magonjwa ya moyo kwa watoto yamegawanyika katika makundi mawili ikwemo magonjwa ya kuzaliwa nayo pamoja na yale yanayotokana na maambukizi.

Hata hivyo amesema kuwa  magonjwa ya moyo kwa Watoto yapo yale ambayo wamezaliwa nayo na yale ya kuambukiza hivyo ni vema wazazi wakafika kupata huduma hiyo mapema kabla tatizo hilo halijawa kubwa.

Mwakilishi  kutoka Taasisi ya I Heart Tanzania,Gedfrey Marlow  amesema lengo la kuweka kambi hiyo kwa mikoa ya Nyanda za juu Kusini Nyanda ni Kuyafikia maeneo ya mikoa saba  ambayo ilikuwa haijafikiwa na huduma hiyo ya upimaji wa moyo kwa watoto ili kutatua changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza kutokana na changamoto ya tatizo hilo kwa watoto.

“Shirika  letu linalenga kutoa matibabu ya Moyo kwa Watoto wote hasa kwa wale waliopo katika maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma hii Muhimu”amesema Marlow

Clara Rweyamamu ni mzazi wa mtoto aliyefanikiwa  kupata huduma hiyo ameishukuru Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya pamoja Taasisi ya 1 Heart Tanzania kwa huduma nzuri alipotiwa katika kambi hiyo ya siku tatu ya upimaji wa moyo kwa watoto.

“Kwakweli najisikia furaha na amani kwa kuwa mtoto wangu hana tatizo lolote baada ya kupima na ninashukuru kwa huduma nzuri zinazotolewa na Taasisi hii “amesema  Rweyamamu.