Na Jackline Martin, TimesMajira Online
SERIKALI imewataka watoa msaada wa kisheria kuwa mstari wa mbele kuwaelimisha wananchi na kuungana na Serikali kutokomeza udhalilishaji, migogoro ya ardhi, pamoja na usajili wa matukio ya kijamii hususani vyeti vya kuzaliwa.
Hayo ameyasema Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla wakati wa kongamano la pili la mwaka la msaada wa kisheria 2022 lililofanyika leo, Zanzibar.
Kongamano hilo lililoenda sambamba na kaulimbiu isemayo ‘Utumiaji sahihi wa njia bora za utatuzi wa Migogoro katika masuala ya msaada wa kisheria Abdulla aliwataka wadau hao kufanya kazi zao kwa uweledi na kwa kuzingatia maadili ili zilete tija na maendeleo yaliokusudiwa.
“Kwa kuwa mnafanya kazi karibu na watendaji wa Serikali za Mitaa wakiwemo masheha basi ni vyema mkashirikiana kwa pamoja kuwasaidia wananchi kupata haki zao,” alisema Abdulla
“Niwatake Masheha na watendaji wengine wa Serikali, muendelee kushirikana na watoaji msaada wa kisheria pamoja na kutambua kazi na juhudi zao kubwa kwani wanafanya kazi bila ya malipo yoyote ila wamejikubalisha kuisaidia jamii.” Aliongeza Abdulla.
Pia Abdulla aliwataka watoaji msaada wa kisheria wote kuendelea kuitumikia jamii kuhakikisha upatikanaji haki na kuendelea kuwa wabunifu katika kuhakikisha taasisi zao zinakuwa na nyenzo za kujiendesha kwa kutafuta miradi mbali mbali badala ya kila siku kusubiri kusaidiwa.
Aidha Abdulla alisema Serikali ya awamu ya nane kupitia uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi imejidhatiti vya kutosha katika kuhakikisha wananchi wake wanapata haki lakini pia wanafata Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 pamoja na Sheria zilizopo.
Pia Abdulla aliwahakikishia watoaji msaada wa kisheria Zanzibar kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na LSF tutahakikisha kwamba watoaji msaada hao wanafanya kazi zao bila ya usumbufu wowote, na kufanya jitahada mbali mbali za kuwasaidia ikiwemo kuwapatia mafunzo mbali mbali kadri hali itavyoruhusu.
“Nafahamu kuwa watoaji msaada wa kisheria mna thamani kubwa nchini na duniani kwa ujumla hivyo kuna haja ya watoaji msaada wa kisheria kuleta ushindani na kuweza kujiendeleza ili kupata ujuzi zaidi.”
Abdulla aliwapongeza LFS kwa kupunguza uhaba wa watoaji wa msaada wa kisheria- Zanzibar.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa LSF, Lulu Ng’wanakilala alisema ili kuhakikisha huduma zinakuwa endelevu LSF imekwisha andaa mpango wa muda mrefu wa kupanua mjadala kuhusu huduma bora na endelevu katika msaada wa kisheria ikiwemo kuwepo kwaMfuko wa msaada wa kisheria, ushirikishwaji wa wadau kuhusu mipango ya Bajeti Wizara ya Katiba na Sheria.
Pia Ng’wanakilala alisema mpango mwingine wa muda mrefu ni Kujenga uwezo wa Idara ya Msaada wa Kisheria, Kuunganisha huduma za msaada wa kisheria katika mfumo wa Serikali za Mitaa na Wasaidizi wa Kisheria kuwa sehemu ya Vituo Jumuishi vya Mahakama.
More Stories
Maghorofa Kariakoo mikononi mwa Tume
ITA chatakiwa kutoa mafunzo ya viwango vya juu na kasi ya maendeleo ya Kisayansi
Wagombea CHADEMA wakipewa ridhaa,watakuwa wawazi