January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watetezi wa haki za binadamu watoa tathimini ya ripoti ya tatu ya mapitio ya haki za binadamu

Na Mwandishi wetu,timesmajira,online

WATETEZI  wa haki za binadamu wameeleza kuwa pamoja na maboresho yanayoendelea kufanyika nchini kwenye masuala ya haki za binadamu, bado kuna changamoto nyingi za kisheria, kisera na mifumo inayoathiri haki hizo kwa baadhi ya maeneo.
Pia wameiomba Serikali kuridhia na kuyakubali mapendekezo yaliyotolewa upya katika Ripoti ya Kikao cha Tatu cha Mapitio ya Hali ya Haki za Binadamu (UPR), 2021 hasa yale yanayogusa haki za msingi za binadamu.


Hayo yamebainishwa juzi  jijini Dar es Salaam na Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa wakati wa kikao cha pamoja cha  THRDC, Kituo Cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Save the Children wakati wakitoa taarifa ya tathmini ya ripoti hiyo ya UPR ya  mwaka huu.


Olengurumu amesema  Serikali inapaswa kuangalia mapendekezo ya umoja wa mataifa  yaliyotolewa upya katika ripoti hiyo hususani zile zinazohusu  haki za msingi, ili iweze kuridhia na kuyakubali kwa kuangalia  maslahi mapana ya watanzania kwa kuwa  haki za binadamu ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa lolote.


Amesema wanaiomba Serikali iwashirikishe wadau wengine wa haki za binadamu hususani Asasi za Kiraia na Nchi wanachama zilizotoa mapendekezo ili kujadili uwezekano wa kuyaboresha kulingana na mazingira halisia ya nchi.


“Tunaiomba Serikali kuridhia mikataba ya kimataifa inayolenga kukomesha vitendo vya utesaji binadamu pamoja na ulinzi dhidi ya kupotezwa, haki za wakimbizi, za watoto kuhusu mabadiliko ya sheria dhidi ya ndoa za utotoni,” alisema na kuongeza

“Nchi wanachama waliotoa mapendekezo pia waangalie uwezekano wa kuyaboresha mapendekezo ambayo hayakukubaliwa na ambayo yanafikiriwa ili yaweze kukubaliwa. Hii ni kutokana na mapendekezo mengi kuunganishwa katika pendekezo moja,” amesema.

 
Aidha amesema UPR ni mchakato unaoendeshwa na serikali za Umoja wa Mataifa kuhakiki hali ya Haki za Binadamu kwa Nchi zote ambazo ni wanachama wa Umoja wa Mataifa.

 
Amesema lengo kuu la utaratibu huu ni kuboresha hali ya Haki za Binadamu katika nchi zote na kushughulikia ukiukaji wa haki za binadamu ili kuifanya dunia sehemu salama kwa kila binadamu. 


“THRDC, LHRC na Save the Children tunaipongeza Serikali ya Tanzania kwa kushiriki kikamilifu katika mchakato huu wa mapitio ya Hali ya Haki za Binadamu tangu mwaka 2011 mpaka sasa ambapo nchi yetu imekua ikiwasilisha ripoti zake kwa wakati na kushiriki katika mchakato wa UPR,” amesisitiza