May 2, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watetezi wa haki za binadamu watoa mapendekezo kwa Serikali sakata la Loliondo

Na Mwandishi wetu,timesmajira,online

WATETEZI wa haki za binadamu nchini wametoa mapendekezo kwa Serikali ambayo wanapaswa kuyafanyia kazi ili kuweza kurejesha amani, utulivu na kutatua mgogoro wa muda mrefu eneo la Loliondo na  Ngorongoro bila ukiukwaji wa haki za binadamu.
Mapendekezo hayo yametolewa jana jijini Dar es Salaam na Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) Onesmo Olengurumwa wakati akitoa taarifa kuhusu ushiriki wa watetezi wa haki za binadamu katika kutatua mgogoro wa ardhi.


Olengurumwa alisema mapendekezo hayo yaliyotolewa kwa serikali ni kuendelea kufanyika kwa majadiliano na maridhiano kati ya wananchi na serikali ili kuondoa taharuki iliyopo. 

Amesema wanaishukuru Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuanza kufungua meza ya majadiliano kupitia kikao kilichofanyika jana tarehe 22 Juni 2022.
“Mapendekezo mengine tunashauri pawe na ushirikishwaji wa kina wa wananchi pamoja na viongozi wao wa kimila na kisiasa katika mipango yote inayoendelea kufanywa katika maeneo hayo,” amesema
Amesema vongozi na wananchi wanapaswa kuepuke kuendelea kutoa kauli za kibaguzi na badala yake waendelee kujenga umoja na kuaminiana katika kutafuta suluhu ya migogoro ya ardhi katika Wilaya ya Ngorongoro.
“Watetezi wa haki za binadamu tunaomba  waendelee kupewa mazingira mazuri ya kazi zao ili waweze kuchangia ipasavyo katika kutatua mgogoro huo,” amesema 
Amesema mtandao huo unashauri serikali kufanya tathmini na kupata idadi kamili ya wananchi waliokimbilia nchi Jirani kwaajili ya matibabu ili angalau waweze kurudi nchini na wahakikishiwe kupatiwa matibabu hapa hapa.
Olengurumea mtandao unashauri Serikali chini ya Uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kuondoa vikosi Loliondo na kurudi kwenye meza ya majadiliano na jamii kuhusu namna ya kuhifadhi maaeneo ya Loliondo. 
“Michakato hii izingatie haki za binadamu na ushirikishwaji mpana wa wananchi ambao ni wakazi wa maeneo hayo. Pia mtandao unashauri viongozi na wananchi waliokamatwa na kushtakiwa waachiwe huru na washiriki katika mazungumzo ya maridhiano.
“Uchunguzi unaofanywa kuhusu kesi ya mauaji ya Askari wa Jeshi la Polisi ufanyike bila kuathiri watu wasiokua na hatia,” amesema 

Naye Robert Kamakia Mkurugenzi Mtendaji Shirika la Kusaidia na Kuinua Maisha ya Wafugaji Tanzania (PALISEP) amesema mgogoro huo umekuwepo kwa muda mrefu na umepelekea ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu hasa kwa wakazi wa Loliondo ikiwemo kuuwawa kwa askari na kupigwa kwa raia, huku baadhi ya wananchi wakikimbilia nchi jirani kwa ajili ya matibabu.
Amesema pamoja na hali hiyo, watetezi wa haki za ninadamu wamekua wakipitia changamoto zinazowarudisha nyuma katika kazi zao ikiwemo kutafsiriwa kama wachochezi wa mgogoro huo.
“Baadhi ya tuhuma hizo zimekua zikitolewa na viongozi wa serikali bila ushahidi wowote unaotolewa kwa umma. Jambo hili limekua na mazara makubwa kwa Watetezi wa Haki za Binadamu ikiwemo kupungua kwa imani ya wananchi kwa watetezi wa haki za binadamu au asasi za Kiraia katika eneo hilo,” amesema 
Awali  Loserian Maoi ambaye pia ni  Mkurugenzi Mtendaji Shirika la Maendeleo Jumuishi Ngorongoro (IDINGO) amesema 
THRDC inaamini kuwa njia bora ya utatuzi wa mgogoro wa Loliondo ni kuwa na majadiliano.
 Amesema wanaishukuru Wizara ya Katiba na Sheria na Idara zote za Serikali zilizoshiriki katika kikao hicho muhimu kama mwanzo wa majadiliano ya kutafuta suluhu ya kudumu katika eneno la Loliondo na Ngorongoro bila ukiukwaji wa haki za binadamu.