December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watetezi wa haki za binadamu watakiwa kufanya kazi kwa pamoja

Na Mwandishi wetu

MKURUGENZI wa Shirika la Mtandao wa Wanawake Duniani, kwa ajili ya utetezi wa haki za afya(WGNRR), Nondo Ejano ametoa wito kwa wadau wanaotetea haki za binadamu hasa wanawake kufanya kazi kwa pamoja ili kuibua sauti zao na changamoto wanazopitia katika jamii zao.

Ejano ametoa wito huo jana jijini Dar es Salaam wakati akifunga warsha ya kuwajengea uwezo  waandishi wa habari katika Masuala mazima ya afya ya uzazi.

Amesema ushirikiano huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kusukuma ajenda mbalimbali kwa serikali na watoa huduma, kufanya marekebisho katika masuala mbalimbali ikiwemo  sheria ya ndoa .

“Leo hii tuna mjadala ambao umekuwa ukiendelea kuhusu sheria hivyo sisi kama wadau ni muhimu kushirikiana kwa kuweka mikakati ya pamoja badala ya kila mtu kufanya kwa namna yake,”amesema.

Ejano amesema kumekuwa hakuna nguvu ya kutosha kwa ajili ya wahanga wote katika jamii, hivyo uwepo wa nguvu ya pamoja utasaidia kupaza sauti ya  pamoja dhidi ya vitendo hivyo.

“Vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu ni vingi kama vile ubakaji, shambulio la kigono  vimekuwa vikisababisha madhara ya kiafya katika maisha wasichana na wanawake kupitia kalamu zenu tunaimani kwa pamoja tutaweza kuibua chagamoto hizo,”amesema.

Amesema kupitia ushirikiano wa pamoja  utasaidia kwa kiasi kikubwa kusukuma ajenda mbalimbali kwa serikali na watoa huduma kufanya marekebisho katika masuala mbalimbali ikiwemo  sheria ya ndoa .

Aidha amefafanua kuwa, Shirika hilo limekuwa likiusika  katika kutetea upatikanaji wa huduma sahihi za stahiki za afya ya uzazi kwa watu wote.

“Tumekuwa tukifanya kazi na jamii lakini kipaumbele chetu zaidi ni wale watu ambao wako katika hali ya chini lengo letu ni kuhakikisha jamii inapata  haki ya kupata huduma stahiki za uzazi wa mpango bila ubaguzi,”amesema.

Kwa upande wake Ofisa Vijana katika Programu za afya ya uzazi(WGNRR), Walta Carlos amesema katika kuchukua hatua thabiti dhidi ya vitendo hivyo ni muhimu kuwepo kwa ushirikiano wa pamoja kwa wadau wote 

Amesema watu wengi wamekuwa wakipaza sauti zao nakusahau watu ambao ni wa muhimu sana katika jamii.

“Katika Masuala haya katika harakati hizi za afya ya uzazi na haki za wanawake na wasichana ni vizuri wadau wote kwa ujumla kushirikiana kwani tunaaamini vyombo vya habari vinaguvu yake pia Taasisi  na Asasi za kijamii nazo zinanguvu yake na hatimaye kutengeneza mkakati wa pamoja ikiwemo kufanya uchambuzi wa baadhi sera,”amesema Walta.