Na Moses Ng’wat,Timesmajiraonline,Mbozi.
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi kuendelea kubuni mambo yatakayoweza kuongeza mapato ya Halmashauri hiyo ikiwemo kuwa na kituo kikubwa cha mabasi na kituo cha maroli.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Mbozi jimboni Vwawa mkoani Songwe akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani humo.
“Mbozi mnaacha pesa inapita inaenda Tunduma, tukiweka kituo hicho Cha maroli tutaona faida yake mtapata mzunguko mkubwa wa mapato”
“Kituo Cha mabasi tuna mabasi yanayoenda Katavi, sumbawanga wametoka Mbeya, hapa lazima ndiyo pawe mahala pa kunywa soda, tutengeneze mazingira hapa iwe mahali pa kula chakula kwa mama lishe na baba lishe” Amesema Waziri Majaliwa na kuongeza kuwa
“Jengeni nyumba za kulala wageni tukishajenga kituo Cha maroli, madereva hawatotaka kulala katika kituo cha magari watataka kulala hotelini hivyo ongezeni nyumba za kulala wageni ikiwemo hoteli za madaraja mbalimbali”
Aidha Waziri Majaliwa amemtaka Meneja Tanesco Mkoa wa Songwe kuweka ratiba ya umeme inayojulikana na kueleweka kwa wananchi ili waweze kuondokana na changamoto hiyo katika maeneo yao.
“Malalamiko ya umeme yapo karibu nchi nzima, muhimu, kuwe na ratiba kwenye maeneo yenu inayosomeka na kujulikana ili wananchi wajue ninj wafanye”
“Sasahivi hatuna shida tuna radio local, tv online, mfumo wa mawasiliano Whatsapp, Instagram, toeni matangazo kupitia vyombo hivyo kutakua na kukatika umeme kwa siku kadhaa ili mtu ajipange, tusije tukaunguza mafriji ya watu, radio za watu, majiko ya watu na nyumba za watu, lazima tujitoe huko” Amesema Waziri
Mbali na hayo, Waziri Majaliwa amesema serikali wanaendelea kuboresha mazingira ya makao makuu katika Mkoa huo wa Songwe ili Vwawa iweze kuwa manispaa ambapo amewaagiza watumishi wa Halmashauri wafanye jitihada ili suala hilo likamilike kwa haraka.
Kuhusu Mbolea, Waziri Majaliwa amesema Rais Samia ameleta mbolea ya ruzuku ambapo amepunguza bei ya manunuzi ya Mfuko wa mbolea kutoka shilingi 120,000 hadi 70,000
“Sasahivi Duniani kote mbolea inapatikana kwa gharama ya juu sana, kwasababu kipindi Cha COVID hakukuwa na biashara ya mazao ya chakula, yanayotoka kwenye nchi Moja mpaka nyingine, kwasababu ya lile zuio hivyo uzalishaji haukuwepo, baada ya COVID uzalishaji umeanza upya Kila Taifa watu wake wanalima sana na sisi watanzania tunalima vilevile kwa maana hiyo mahitaji ya mbolea yamekuwa makubwa , Makampuni ya mbolea yamezidiwa na oda na Kila kampuni Ina mataifa rafiki na kwenye biashara kubwa kuliko nchi ambazo Zina biashara ndogo”
“Sisi watanzania tunahitaji mbolea Tani laki 7 tu hivyo tunalazimika kununua bei za juu tukileta mbolea Tanzania tunaiuza mfuko mmoja kilo 50 shilingi 120,000 ambayo watanzania hawana uwezo wa kuinunua, mhe. Samia amelijua hili akatafuta utaratibu wa kuwaongezea Kila Mtanzania anayenunua mfuko wa mbolea ili anunue bei ya chini nyingine zilipie serikali ,hivyo mfuko wa 120,000 sasa utanunua kwa 70,000 na 50,000 zinalipwa na serikali”
More Stories
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake