Na Steven Augustino, TimesMajira Online,Tunduru
WATU watatu katika vijiji vya Mtonya katika Kata ya Mindu na Tulieni Kata ya Nakapanya wilayani Tunduru mkoani Ruvuma wamefariki dunia baada ya kukanyagwa na tembo, baada ya wanyama hao kuvamia kwenye maeneo ya vijiji vyao.
Aidha, katika tukio hilo pia mkazi wa Kijiji cha Mtonya aliyetambulika kwa jina la Zuberi Wakati Mchopa (70)amelazwa katika hospitali ya serikali ya Wilaya ya Tunduru kwa matibabu baada ya kujeruhiwa vibaya na wanyama hao.
Afisa Wanayamapori wa Wilaya ya Tunduru, Limbega Hassan Ally amesema kuwa, matukio hayo yalitokea kwa nyakati tofauti Novemba 9, mwaka huu na kwamba baada ya kupokea taarifa hizo tayari amekwishapeleka askari wenye silaha kwa ajili ya kuwafukuza tembo hao ili wasiendelee kuleta madhara kwa wananchi.
Limbega amewataja waliofariki katika matukio hayo kuwa ni Jamira Mathayo Mchopa (47) mkazi wa Kijiji cha Tulieni Kata ya Nakapanya wilayani humo ambaye tukio la kushambuliwa kwake lilitokea majira ya saa 10:00 asubuhi akiwa shambani kwake.
Limbega amemtaja mtu mwingine aliyefariki katika matukio hayo kuwa ni Jastini Gideon Mchopa (54) mkazi wa Kijiji cha Mtonya katika Kata ya Mindu ambaye tukio la shambulio hilo lilitokea majira saa 9:30 wakati akiwa shambani.
Kwa mujibu wa Limbega mtu mwingine aliyepoteza maisha katika matukio hayo alitambulika kwa jina la Stephano Hassan Joseph (78) mkazi wa Kijiji Mtonya katika Kata Mindu ambaye alishambuliwa majira ya saa 8:00 asubuhi akiwa shambani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Simoni Msigwa amethibitisha kuwepo kwa matukio hayo na kwamba polisi wanaendelea na uchunguzi wa chanzo cha vifo vyao.
More Stories
Jokate awapa tano vijana UVCCM maandalizi Mkutano Mkuu wa CCM
Watakaokwamisha mapato Kaliua kukiona cha moto
Dkt.Gwajima aagiza kuundwa kamati za ulinzi wa watoto