Na Moses Ng’wat, Timesmajira Online,Songwe
POLISI Mkoani Songwe wanawashikilia wanaume watatu wote raia wa Tanzania na wakazi wa Wilaya ya Mbozi, wakituhumiwa kukutwa na vipande tisa vya meno ya Tembo vyenye uzito wa kilo 20 bila kuwa na kibali.
Akitoa taarifa za kukamatwa kwa nyara hizo za serikali Februari Mosi 2024, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Gallus Hyera, amesema watu hao walikamatwa kati ya Januari 30 na 31, 2024 huko katika kijiji cha Ibembwe, Kata ya Igamba, wilayani Mbozi, wakiwa katika harakati za kutafuta wateja.
Hata hivyo, Kaimu Kamanda Hyera hakuweza kutaja majina ya watuhumiwa hao kwa maelezo kuwa bado jeshi hilo linaendelea na uchunguzi ili kubaini mtandao wote unaojihusisha na vitendo hivyo vya ujangili.
“Uchunguzi wa awali umebaini kuwa watuhumiwa ni sehemu ya mtandao wa watu wanaojihusisha na shughuli za uwindaji haramu, usafirishaji na uuzaji wa nyara za serikali hivyo majina yao tunahifadhi hadi hapo upelelezi wetu utakapokamilika na hatimaye kuwafikisha mahakamani,” amefafanua Kaimu Kamanda Hyera.
Kaimu Kamanda Hyera amebainisha kuwa kukamatwa kwa watuhumiwa hao kumetokana na taarifa za siri ambapo baada ya kukamatwa na kupekuliwa watuhumiwa walikutwa na nyara hizo za serikali zikiwa zimefichwa kwenye begi na kisha kutumbukizwa kwenye mfuko wa sandarusi.
More Stories
Wakuu wa Wilaya,Wakurugenzi watakiwa kusimamia programu za chakula shuleni
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito