Na Penina Malundo,TimesMajira Online,Kagera
MGOMBEA urais kwa CCM, John Magufuli amewasili mkoani Kagera jana na kupokelewa na maelfu ya wananchi na kuwataka Watanzania kutochagua watu wasioaminika watakaokuja kutawala kwa matakwa ya watu wengine.
Pia amesema atakapomaliza kipindi cha miaka yake 10 ya uongozi, hatataka kuongeza tena muda bali watapatikana wengine ndani ya Chama hicho.
Rais Magufuli alitoa kauli hiyo akiwa njiani kuelekea mjini Bukoba, kwa ajili ya kuendelea na mikutano yake ya kampeni mkoani Kagera.
Dkt.Magufuli alisema ni vema Watanzania wakachagua watu ambao hata wakiambiwa fanyeni hivi, wana uwezo wa kuwaambia hawawezi kufanya.
Alisema kazi ya uongozi haihitaji kujifunza, bali inatakiwa kuwajali watu, kujituma na kumtanguliza Mungu.
“Tuachane na propaganda zinazofanyika kwamba wakichaguliwa wao watafuta kodi kitu ambacho ni kigumu. Wanasema wakichaguliwa watafuta kodi wakati katika mikutano yao wanachangisha kodi,”alisema Dkt. Magufuli na kuongeza;
“Unasema utafuta kodi ,ukienda katika mikutano unaomba kuchangiwa,sasa wakiingia zile tulizozikusanya si watazitumia vibaya, zile tulizopanga kununua meli, umeme, kutengeneza miundombinu mbalimbali kama barabara na reli ya umeme si zitapotea?”
Alisema kiongozi lazima ajikubali moyoni mwake kwa ajili ya kuwatumikia maskini, hawatapata serikali ya kuwagawia pesa kwani hata maandiko ya vitabu vya dini hayasemi hivyo.
“Mara mnaambiwa hamna kulipa kodi,mtaendesha nchi bila kulipa kodi,hata Ulaya wanalipa kodi,”alisema na kuongeza;
“Muepuke watu wenye tamaa ya kura kwa kuwadanganya,Watanzania mjitambue,”alisema Dkt.Magufuli
***Miaka 10 ya uongozi wake
Dkt.Magufuli alisema akimaliza miaka yake mitano ijayo, hataki kuongeza muda hivyo watapatikana watu wengine ndani ya chama chao ili waongoze.
Alisema kipindi hicho kikifika yeye atapumzika na kuangalia wenzake wanavyofanya kazi. “Palikuwepo na Baba wa Taifa,Mwl Nyerere alifanya miaka yake akapumzika, akatutoa kwenye ukoloni ,akaja Mzee Mwinyi naye akaendelea na ruksa akafanya kazi yake katika miaka kumi angeweza kuendelea lakini alisema imetosha,”alisema na kuongeza;
“ Mzee Mkapa naye amemaliza miaka yake 10 akapumzika,amekuja Mzee Kikwete amefanya kazi yake miaka kumi amepumzika ,mimi nimekuja nimefanya miaka mitano ndio maana naomba niongezewe miaka mitano ile iliyobaki nikafanye maajabu kwa ajili ya maendeleo ya nchi hii.”
***Prof. Anna Tibaijuka
Dkt. Magufuli alisema miaka mitano iliyopita alipita Wilaya ya Muleba kuomba kura kwa heshima kubwa akiwa na mgombea ubunge wakati huo, Prof. Anna Tibaijuka.
Alisema Prof.Tibaijuka ni dada yake tangu alipokuwa Naibu Waziri wa Ujenzi na akiwa Mbunge wa Chato, huku mume wa Prof.Tibaijuka akiwa Balozi wa Sweden.
“Mama Tibaijuka amesema amestaafu, lakini kwangu mimi hajastaafu, hii ndiyo faida ya kuwa na watu katika mahali fulani ambapo wanaweza kusaidia Serikali,”alisema na kuongeza;
Katibu Mkuu wa CCM,Dkt.Bashiru Ally hakutegemea kuwa katibu Mkuu wa chama chetu kwa nchi nzima, kwani alikuwa anauza ndizi pale Kemondo baadaye alienda chuo kikuu kufundisha, lakini leo ndio kawa katibu Mkuu wa CCM Tanzania nzima.
“Serikali ina mavyeo mengi,mimi namwambia Prof.Tibaijuka hajastaafu licha ya kusema amestaafu, hatuwezi kumuacha Prof.Tibaijuka anakaa wakati kuna maeneo mengi anaweza kwenda kufanya.”
***Mgombea Ubunge wa Jimbo la Muleba
Dkt.Magufuli alisema wana Muleba wanatakiwa kuwa kitu kimoja, tayari chaguzi ya ndani ya Chama imefanyika na kwa bahati nzuri waliojitokeza watu wengi katika kugombea nafasi ya ubunge kwa jimbo hilo.
“Tunatakiwa sisi wana Muleba tuwe kitu kimoja tumefanya chaguzi ndani ya chama, walijitokeza wengi ,sisi chama tulichambua aliyeongoza na aliyekuwa wa pili hadi wanne tunawafahamu tukaona yupo ambaye ni mzuri zaidi.”
Aidha akizungumzia suala la kuondoa umaskini katika Wilaya ya Muleba, Dkt. Magufuli alisema kupitia mradi wa TASAF imeletwa bilioni 12.6 na mpango huo utaendelea.
“Tumesimama hapa kuomba kula,tunaamini kupitia ilani ya uchaguzi ambayo mambo mengi yameelezwa ya Muleba na Tanzania kwa ujumla katika ilani yetu kitabu kina ukurasa 303 ,”alisema na kuongeza
More Stories
Watoto wenye uhitaji wapatiwa vifaa vya shule
Wananchi Kisondela waishukuru serikali ujenzi shule ya ufundi ya Amali
RC.Makongoro ataka miradi itekelezwe kwa viwango